Idadi vifo ajali ya mafuta yafika 93

17Aug 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Idadi vifo ajali ya mafuta yafika 93

IDADI ya watu waliopoteza maisha kutokana na ajali ya lori la mafuta mkoani Morogoro imeongezeka na kufika 93 baada ya majeruhi wengine wanne waliokuwa wamelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufariki dunia jana.

Kufuatia vifo hivyo, idadi ya wagonjwa waliobaki katika hospitali hiyo kubwa zaidi nchini ni 25 kati ya 46 waliokuwa wamefikishwa kupatiwa matibabu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alitoa taarifa hizo jana alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutembelea hospitali hiyo kuona majeruhi hao.

Alisema wagonjwa wengine 21 wanaoendelea kupatiwa matibabu Muhimbili wamewekwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU).

Alisema madaktari wanafanya kila jitihada kuokoa maisha ya wagonjwa waliobaki ili wapone na kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Ummy alisema ili kuhakikisha wagonjwa hao wanapata huduma bora, kila mgonjwa ana nesi wake anayemtazama kwa karibu.

Waziri huyo pia aliagiza kuanzishwa kwa kitengo maalum cha kuhudumia wagonjwa wanaotokana na ajali za moto kitakachokuwa na chumba cha wagonjwa mahututi.

Alisema kuwapo kwa kitengo hicho kutasaidia wagonjwa wanaopata ajali za moto kupata huduma za matibabu kwa wakati na haraka.

Mkuu wa Kitengo cha Dharura cha MNH, Dk. Charles Majinge, alisema wagonjwa wanapewa huduma inayotakiwa na wote waliobaki wamewekwa ICU.

Alisema wagonjwa hao wamewekwa ICU ili kuongeza umakini wa juu zaidi katika kuwahudumia.

Idadi hiyo ya waliopoteza maisha inatokana na ajali ya lori lililokuwa limebeba tangi la mafuta ya petroli, kuanguka eneo la Msamvu mkoani Morogoro na baadaye kulipuka wakati baadhi ya wananchi wakichota mafuta yaliyokuwa yanamwagika.

Habari Kubwa