Waziri aagiza wadaiwa sugu ardhi wakamatwe

17Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
SIKONGE
Nipashe
Waziri aagiza wadaiwa sugu ardhi wakamatwe

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula, ameiagiza idara ya ardhi katika Halmashauri ya Sikonge mkoani Tabora kuhakikisha inawafikisha kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi wa wilaya hiyo wanaodaiwa takriban Sh. milioni 150

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula

Dk. Mabula alitoa agizo hilo juzi katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi na kukagua masjala ya ardhi na mifumo ya ukusanyaji kodi kwa njia ya kielektroniki mkoani Tabora.

Dk. Mabula alieleza kushangazwa na idara ya ardhi katika halmashauri hiyo kushindwa kuwafikisha wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba wakati sheria inaelekeza baada ya siku 14 mdaiwa asipotii wito, afikishwe katika baraza hilo.

Alibainisha kuwa katika Halmashauri ya Sikonge kuna baadhi ya wamiliki wa ardhi ambao kwa mara ya mwisho walilipa kodi ya ardhi mwaka 2000, lakini idara ya ardhi imeshindwa kuwadai ama kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Kaimu Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Martin Ukongo, alisema ofisi yake tayari ilishasambaza ilani 105 kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka huu lakini baadhi yao hawajafikishwa kwenye Baraza la Ardhi.

Dk. Mabula pia aliiagiza halmashauri hiyo kupitia idara ya ardhi kuhakikisha inapima mashamba yote yaliyoko katika halmashauri hiyo, akibainisha kuwa kutopimwa kwa mashamba hayo kunatoa fursa kwa wamiliki wake kutolipa kodi ya ardhi.

''Sikonge mna mashamba hayajapimwa wakati ni ya wafanyabiashara wakubwa, hapa wanakwepa kulipa kodi, 'why' (kwanini) hamjawapimia na kuwapatia hati ili walipe kodi?" Dk. Mabula alihoji.

Mkuu wa Kitengo cha Kodi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami, alisema wizara sasa imeimarisha mfumo wa ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa kurahisisha ukadiriaji na kufanya malipo kupitia simu ya mkononi.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Peres Magiri, alimweleza Dk. Mabula kuwa katika mwaka uliopita, wilaya yake ilifanikiwa kukusanya kodi ya pango la ardhi Sh. milioni 29.127, sawa na asilimia 87.55 ya lengo la kukusanya Sh. milioni 33.2.

Magiri alisema wilaya yake imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kama vile kutoa matangazo na kuelimisha jamii kupitia mikutano.

Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM), alimpongeza Dk. Mabula kwa kufanya ziara katika wilaya hiyo, akibainisha kuwa amekuwa kiongozi wa kwanza wa wizara hiyo kuitembelea wilaya hiyo toka ianzishwe.

Kakunda alisema wilaya hiyo iko nyuma katika Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi na kuomba wizara kuipa kipaumbele katika upimaji ili kuepusha migogoro ya ardhi hasa ile ya wakulima na wafugaji.

Habari Kubwa