Polisi wanaowakwaza watalii kushughulikiwa

17Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Polisi wanaowakwaza watalii kushughulikiwa

SERIKALI imesema itaendelea kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya utalii ikiwamo ya polisi kusimamisha magari yenye watalii mara kwa mara.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, aliyasema hayo juzi alipozungumza na wadau wa utalii nchini katika kongamano la utalii lililofanyika mkoani Arusha.

Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau wa utalii nchini imejenga vituo vya ukaguzi wa magari ya utalii ili kupunguza usumbufu kwa watalii barabarani.

Alisema vituo hivyo vitashughulikia masuala ya msingi ikiwa ni pamona na suala madereva wa magari yanayobeba watalii kupimwa kilevi.

Alisema mbali na kilevi, vituo hivyo vitashughulikia vitendo vyote ya uhalifu watakavyofanyiwa watalii.Kanyasu alisema lengo la serikali ni kupunguza kero kwa watalii ili nchi ifikie lengo la kupata watalii milioni mbili mwaka huu.

Alisema licha ya kujengwa vituo hivyo vya ukaguzi, bado kuna kero ambazo zinafanyiwa kazi lengo ili kuboresha sekta ya utalii nchini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, aliwataka wadau wa utalii kufuata sheria, huku akitoa rai kupewa taarifa za polisi wanaowakwaza watalii."Nipigieni simu hata saa nane za usiku kwa askari wanawaomba rushwa nishughulike nao," Shana alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema lengo la Arusha kuanzisha vituo vya ukaguzi magari ni kupunguza kero.

Alisema wanaamini uwapo wa vituo hivyo utafanya mazingira bora kwa watalii na wafanyabiashara.Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Watalii (Tato), Wilbard Chambulo, alisema ujenzi wa vituo hivyo ni hatua muhimu kuwahakikishia watalii usalama wao pindi wakiwa barabani.

Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda, alisema Mkoa wa Arusha ni mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine kwa kujenga vituo hivyo.

Habari Kubwa