Simba, Yanga maneno makali hayavunji mfupa

17Aug 2019
Barnabas Maro
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba, Yanga maneno makali hayavunji mfupa

MANENO tu hayawezi kuvunja mifupa hata yakawa makali kiasi gani. Methali hii hutumiwa na mtu anayepuuza maneno yaliyosemwa na mtu mwingine na ambayo hayawezi kumdhuru kwa namna yoyote au hayamzuii kutekeleza atakalo.

Hakuna mpiganaji anayekwenda kupambana akisema atashindwa. Lazima atoe maneno ya vitisho dhidi ya mpinzani wake ili kumwogopesha na kumkatisha tamaa.

      Jambo hili lanikumbusha vita vya (si vita ‘ya’) Kagera. Aliyekuwa Rais wa Uganda, Jenerali Idi Amin ‘Dada’ (Mungu amrehemu) alijitapa sana kuwa ndege zake za kivita zingeweza kulishambulia jiji la Dar es Salaam na kurejea Uganda katika muda wa dakika tano!

       Aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati ule, Mwalimu Julius Nyerere (Mungu amrehemu), hakutaka vita bali alipenda mapatano ingawa askari wa jeshi la Uganda walikwisha ingia mkoani Kagera nchini Tanzania kwa madai kuwa ni ‘eneo la Uganda!’

Vitisho vya Idi Amin ‘Dada’ wakati askari wake wakiwa tayari wameingia Tanzania kupitia Kagera na kuharibu daraja linalozitenganisha Uganda na Tanzania, vilimlazimu Mwalimu Nyerere aamuru majeshi ya Tanzania kwenda kukomboa ardhi ya Tanzania iliyokaliwa na wavamizi.

Mwalimu Nyerere alisema: “Tutampiga Idi Amin. Sababu tunazo, nia tunayo na uwezo tunao.” Kuanzia hapo askari wakakamavu wa Tanzania wakaingia vitani, wakawafurusha (fukuza watu au wanyama) wanajeshi wa Uganda, kuwaua na kuteka baadhi ya vifaa vyao vya vita walivyoviacha nyuma kukimbia mashambulizi.

Hata wanajeshi wa Libya waliopelekwa Uganda kuisaidia, hawakufua dafu kwa majeshi ya Tanzania. Aliyekuwa kiongozi wa Libya ambaye sasa ni marehemu, alimwomba Rais Nyerere awaachie askari wake na angekuwa tayari kuipa Tanzania fungu kubwa la hela. Mwalimu Nyerere alikataa akisema hafanyi biashara ya kuuza binadamu; akawaachia bila malipo, wakarejea kwao.   

Jenerali Idi Amin ‘Dada’ alikimbia baada ya kusikia wanajeshi wa Tanzania wameingia Uganda. Akaikimbia nchi yake na kusahau bastola yake chumbani! Alifia ughaibuni kwa Waarabu.

Wahenga walisema: “Mwenye kelele hana neno.” Aghalabu mtu anayepiga kelele huwa hana madhara yoyote. Methali hii hutumiwa kutukumbusha kuwa hatupaswi kumwogopa mtu mwenye kelele au fujo kwani kwa kawaida hana neno.

Pia ilisemwa kuwa “Msi hadhari hujifunga kwa ulimi wake.” Asiyetahadhari katika usemaji wake huenda akajitosa taabani kutokana na asemayo. Methali hii yatunasihi tusiwe na tabia ya kupayukapayuka bila ya kuyazingatia, kuyapima na kuyatathmini tuyasemayo hasa katika kadamnasi (hadharani; jahara).

Kuna wakati timu za Simba na Yanga huponzwa na sifa za magazeti yetu ya michezo. Umwambiapo mwenzako ‘nitakupiga,’ kwa mtu jasiri maana yake unamwambia ajiandae kwa vita. Wakati wewe uliyemtahadharisha mpinzani wako, unapoingia vitani kwa mbwembwe, mpinzani wako ataingia kwa tahadhari na nguvu na hatimaye kukushangaza. Unaposhangaa, yeye atajitahidi kukupiga na ikishindakana, wote mtarudi nyuma kama majogoo wanaoogopana!

Michezo ya hivi karibuni ya kimataifa, Simba ilipambana ugenini dhidi ya UD do Songo ya Msumbiji na matokeo kuwa suluhu ya kutofungana. Yanga ilikuwa nyumbani kupimana ubavu na Township Rollers ya Botswana na kufungana 1-1 Yanga ikisawazisha kwa penalti, wakati Azam ikiwa ugenini Ethiopia ikipoteza mchezo kwa kufungwa na timu ya Fasil Kenema bao 1-0 na KMC ikitoka suluhu ugenini Rwanda dhidi ya AS Kigali.

      Nathubutu kusema suluhu, sare na kushindwa kwa timu nilizozitaja kumesababishwa na sifa za magazeti ya michezo nchini. Badala ya kuzihimiza timu hizo kucheza kwa tahadhari na bidii, yalizisifu mno na kuwavimbisha vichwa baadhi ya wachezaji kuwa hakuna timu za kuwashinda! Hakuna timu inayocheza ili ishindwe kwani kila moja ina nia ya ushindi.

      Sasa soma vichwa vya habari za magazeti ya michezo: “Mtakoma! Simba mpya ni krosi, kona, bao.” “HAMTAAMINI Jeshi tayari kwa vita, MO apewa jeuri mpya.” “MO Banka, Sibomana mtapata tabu sana.” Vichwa vya habari kama hivi ndivyo vinavyowaponza wachezaji wetu wakiamini kushinda tu kana kwamba wapinzani wao hawataki ushindi!

      Unapomtisha mpinzani wako kwa maneno kuwa utampiga, maana yake ni kumzindua ajiandae kupigwa. Hivyo hujiandaa hasa kwa lengo na nia ya kukushinda wewe unayetamba kumpiga.

      Nadhani ni bora magazeti yetu yawahimize wachezaji wa timu zetu kufanya mazoezi magumu na kuwa na mbinu (si ushirikina wala rushwa) za kisasa ili kuzishinda timu ngeni. Wanachama na mashabiki hupata wakati mgumu sana timu zao zinaposhindwa nje ya nchi na wakati mwingine hata nyumbani! Matokeo yake ni idadi ya wanaokwenda uwanjani kuzishangilia timu zao kupungua hivyo timu huathirika kimapato.

      Twapaswa kutambua tofauti ya ‘utani’ na ‘uadui.’ Maana ya ‘utani’ ni taratibu au desturi za kimila zinazowafanya watu wanaojuana waweze kuambiana au kutendeana jambo lolote la mzaha bila ya kuleta chuki au kero; dhihaka. Ni tabia ya watu kufanyiana masihara kwa lengo la kuambiana kweli na kuimarisha uhusiano wao.

      Kuambiana ukweli hakufanywi wakati mwenzako anaadhibiwa uwanjani bali kinachotakiwa ni kumhimiza ili ajitahidi na kumpa maneno ya faraja (utulivu wa moyo). Kumzomea mtani wako wakati anapigwa na mgeni, ni kuzidi kumvunja nguvu huku mgeni akipata ahueni na nguvu zaidi. Huo si uzalendo bali ni ujinga, yaani hali ya mtu kutojua jambo fulani; ubwege.

      ‘Uadui’ ni hali ya kutokuwapo maelewano baina ya watu; watu kuchukiana na kutendeana maovu; uhasama. Kwa nini watu wa nchi moja na jiji moja wawekeane upasi (hali ya kutopendana)? Ndivyo tulivyo wanachama na mashabiki wa Simba na Yanga!

Habari Kubwa