Ramaphosa atangaza neema kwa Tanzania

17Aug 2019
Gwamaka Alipipi
Morogoro
Nipashe
Ramaphosa atangaza neema kwa Tanzania

AFRIKA Kusini imeendelea kutoa neema kwa Tanzania baada ya jana Rais wake, Cyril Ramaphosa, kuahidi kukifanya kituo cha utalii kilichokuwa kituo cha ukombozi kwa wapigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika cha Solomon Mahlangu kilichoko katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro

Rais Cyril Ramaphosa.

Vilevile, ameahidi wanafunzi na walimu walioko katika Shule ya Sekondari Chief Albert Luthuli iliyoko kwenye kituo hicho, kushirikiana kielimu na mojawapo ya shule za sekondari za Afrika Kusini kwa lengo la kuendeleza undugu uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Ramaphosa alitangaza neema hiyo jana mkoani Morogoro alipotembelea kituo hicho kilichoko eneo la Mazimbu kilichotumiwa na wanaharakati kudai uhuru na kukomesha vitendo vya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.

"Kuna haja kwa serikali za nchi ya Tanzania na Afrika Kusini kushirikiana kwa pamoja katika kuliendeleza eneo hili, mazao yanayozalishwa katika Mkoa wa Morogoro kuuzwa Afrika Kusini, hivyo hivyo kwa bidhaa za Afrika Kusini kuuzwa Tanzania," Ramaphosa alisema.

Alisema serikali za Tanzania na Afrika Kusini zinapaswa kuhakikisha zinaimarisha miundombinu ya eneo hilo na kutoa ajira kwa wakazi wanaolizunguka.Rais Ramaphosa alisema Kituo cha Solomon Mahlangu kinaendelea kukumbukwa na wananchi wa Afrika Kusini kwa kuwa ndiyo mikakati ya ukombozi wa taifa lao ilikuwa ikipangwa.

Alisema kuwa mbali na kusaidia Afrika Kusini, eneo hilo pia limevisaidia vyama vingi vya siasa vya nchi za Afrika kama vile Frelimo, Zanu, Swapo na ANC katika harakati za kudai uhuru.

"Hii ni mara yangu ya kwanza kufika Morogoro hususan eneo hili la ukombozi, japokuwa kaka yangu alikuwa anaishi hapa, ninajisikia furaha kufika eneo hili, nimekuja kwenye eneo ambalo kwa miaka ya nyuma lilitoa malazi kwa wapigania uhuru wetu, wengine walikuja wakiwa watoto, wengi walizikwa hapa," Rais Ramaphosa alisema.

Aliongeza kuwa ni vema kwa Tanzania na Afrika Kusini kuendelea kushirikiana katika masuala ya kiuchumi, teknolojia na ujuzi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, alisema Tanzania iko tayari kufundisha lugha ya Kiswahili Afrika Kusini.

Alisema eneo la Solomon Mahlangu limeunganisha undugu wa Tanzania na Afrika Kusini na kwamba Serikali ya Tanzania iliyakarabati majengo yake ili kuimarisha na kuwakumbuka wapigania uhuru.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema: "Kituo cha Solomon Mahlangu ni sehemu ya Afrika Kusini."

Habari Kubwa