Waamuzi sawa waadhibiwe, lakini walipwe kwa wakati

19Aug 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waamuzi sawa waadhibiwe, lakini walipwe kwa wakati

KABLA msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara wa 2019/20 haujaanza, tayari waamuzi watakaochezesha wamepigwa mkwara kuwa yeyote atakayeonekana kuchezesha vibaya, au kwenda kinyume na sheria za soka, basi ataondolewa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Salum Chama, amesema kuwa wameweka sheria kali ya kuwabana waamuzi kwa msimu ujao, ambapo watakuwa wanafuatilia kuanzia mechi ya kwanza na atakayebainika kwenda kinyume watamwondoa haraka.

“Hatutamvumilia mwamuzi atakayekwenda kinyume cha kanuni, yapo makosa ya kibinadamu yanaweza kutokea, lakini tukibaini mwamuzi amepindisha sheria, huku akifahamu, tutamfuta moja kwa moja," anasema na kuongeza.

“Mfano kuna mambo ya kukataa bao ambalo ni halali, au kutoa kadi kwa mchezaji asiyestahili, kwa kweli mwamuzi kama huyo mara moja tutaanza naye, lengo ni kuboresha sekta hii,” anasema.

Hili ni jambo ambalo litawafanya sasa waamuzi wawe makini wanapokuwa wanachezesha soka, lakini pia watakuwa wakitoa maamuzi sahihi na kuachana na maamuzi tata ambayo mashabiki wengi wanakuwa na tafsiri kuwa amechukua rushwa, au ana mapenzi na timu fulani.

Ukweli ni kwamba klabu zinajiandaa kukaa kambini, zinaingia gharama kubwa kuwa na wachezaji bora, kuwalipa vizuri, lakini mwamuzi mmoja anaingia na matokeo yake mfukoni, akitaka kufanya kila hila ili timu yenye uwezo isiibuke na ushindi.

Hapo ndipo huwa tunaona vituko baada ya vituko. Lakini pia Chama aangalie upande wa pili kama waamuzi hao wanalipwa stahiki zao vema, ili kutoingia kwenye ushawishi wa kupanga matokeo.

Kuna taarifa kuwa waamuzi wengi wamekuwa wanacheleweshewa stahiki zao. Vile vile inaelezwa kuwa waamuzi wengi huwa wanakwenda kuchezesha vituoni wakitumia nauli zao na kukaa hotelini kwa gharama zao na wanafanya hivyo hadi pale watakapokuja kulipwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Hali kama hii inakaribisha kabisa harufu ya rushwa kwani kama timu mwenyeji ikiamua kumgharamia mwamuzi au waamuzi hao hoteli na chakula tu, achilia mbali pesa ya mfukoni, basi anaweza kuwakirimu kwa kuwachezesha kwa upendeleo.

Mimi nadhani kabla ya mkwara huu, Chama angewaambia waamuzi wote kuwa kuanzia sasa watalipwa kwa wakati posho zao, hivyo hakuna kisingizio chochote, atakayevurunda cha moto atakiona.

Sina maana kuwa kwa sababu mwamuzi anacheleweshewa stahiki zake, basi ndiyo afanye madudu, lakini hii itamfanya asiwe na kisingizio kuwa labda alikuwa na msongo wa mawazo kutokana na kutokuwa na pesa mfukoni.

Waswahili wanasema haki na wajibu, waamuzi wanaweza kuwa na visingizio tele kama wataendelea kukopwa na wanaweza kuwa na watetezi, lakini kama wakilipwa vizuri na kwa wakati sidhani kama kutakuwa na mtu anayeweza kuwa na huruma nao kama wakivurunda mechi yoyote ile.

Lakini pia waamuzi hawa wasiwe wanafungiwa au kuondolewa kwenye ligi kwa shinikizo la mitandao ya kijamii.

Kumezuka tabia ya mihemko ya mashabiki hasa wa timu kubwa kushinikiza waamuzi wapewe adhabu hata kama kosa lenyewe ni la bahati mbaya au la kibinadamu.

Na waamuzi wanaopata matatizo hayo mara nyingi huwa ni wale wanaozichezesha timu kubwa za Simba, Yanga na Azam. Cha ajabu kuna baadhi ya malalamiko kutoka kwenye timu zingine, lakini kwa sababu ni mechi ambazo hazizihusu klabu hizo kubwa, basi waamuzi hawachukuliwi hatua yoyote.

Mwenyekiti huyo pia anapaswa aziangalie zaidi mechi ambazo hazionyeshwi laivu kwenye televisheni. Uchunguzi wangu mdogo tu unaonyesha kuwa baadhi ya mechi chache ambazo hazionyeshwi zinakuwa na matokeo yenye utata mkubwa na malalamiko kuwa waamuzi wanafanya chochote wanachojisikia kwa sababu hawaonekani.

Mechi kama hizi hata kama hazionyeshwi, zinapaswa ziangaliwe kwa jicho la tatu kwa kutuma waangalizi ambao watapeleka taarifa moja kwa moja kwenye kamati hiyo. Yangu ni hayo tu katika hilo.

Habari Kubwa