Serikali iendeshe operesheni ya kusomba pamba ya wakulima

20Aug 2019
Raphael Kibiriti
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serikali iendeshe operesheni ya kusomba pamba ya wakulima

NIANZE kama Mtanzania kuipongeza serikali kwa kufanikisha kwa kishindo Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), uliohitimishwa juzi jijini Dar es Salaam.

Ni bayana kwamba mkutano huo umeongeza alama kwa taifa na hasa baada ya lugha adhimu ya Kiswahili kupitishwa kuwa miongoni mwa lugha rasmi nne zinazotumika SADC, zikiwamo za Kingereza, Kifaransa na Kireno.

Lakini pia umeongeza alama kwa nchi baada ya Rais John Magufuli kuchukua mikoba ya uongozi wa Jumuiya kutoka kwa Rais wa Namibia, Dk. Hage Geingob.

Nimeona leo niendeleze ajenda ya ununuzi wa pamba ya wakulima, kwani bado utatuzi wake haujawa katika kiwango cha kuridhisha.

Hali iko hivyo kwa mujibu wa taarifa alizonazo Muungwana kutoka maeneo mbalimbali yanayolima pamba, hasa Kanda ya Ziwa pamoja na ahadi aliyoitoa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye sherehe za Nanenane.

Akiwa kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Nanenane kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu, Agosti 8, Majaliwa aliwahakikishia wakulima wa zao hilo kuwa pamba yote itanunuliwa na kuondoka mikononi mwao.

Aidha, akazitaka benki zote zinazotoa fedha kwa kampuni za ununuzi kutoa taarifa kwa serikali kiasi cha fedha walizotoa kuwawezesha wakuu wa mikoa na wilaya kuweka mikakati ya usimamizi ili fedha hizo zipelekwe kwenye ununuzi wa zao hilo na si vinginevyo.

Nia ya maelekezo hayo kwa mujibu wa Majaliwa ni kuhakikisha pamba yote inatoka mikononi mwa wakulima, wanapata fedha zao na hatimaye wajiandae kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo na maboresho ya shughuli zao za kimaendeleo.

Hata hivyo, ikiwa ni takribani wiki mbili sasa toka maagizo hayo yatolewe, bado hali kwenye vyama vingi vya msingi vya ushirika (AMCOS), iko vilevile.

Bado maghala ya AMCOS yamejaa huku pamba nyingine ikiwa imehifadhiwa nje na hasa katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga.

Bado wakulima walio wengi waliopeleka pamba yao kwenye maghala ya AMCOS, hawajalipwa fedha zao.

Maagizo ya serikali kwamba pamba hiyo iwe imesafirishwa kwenda viwandani ili nafasi ya kuhifadhi pamba ambayo bado iko mikononi mwa wakulima ipatikane, hayajatekelezwa.

Muungwana ana taarifa kwamba bado kampuni za ununuzi hazijapeleka magari ya kusomba pamba, kutoka kwenye maghala ya AMCOS hadi sasa.

Aidha, taarifa zinabainisha kwamba kuchelewa kwa wanunuzi wa zao hilo kutekeleza agizo la serikali pengine linatokana na ukweli kwamba baadhi ya wakulima waliamua kuingia gharama za kupeleka wenyewe pamba kwenye viwanda ili ikanunuliwe.

Na ndiyo maana kwa mfano maghala ya viwanda vya pamba vilivyoko Shinyanga, yalikuwa yamejaa kiasi cha nyingine kuwekwa nje.

Hatua hii ya wakulima kuamua kupeleka pamba yao wenyewe kwenye viwanda bila ya kupitia AMCOS, kimsingi ndiyo ambayo imesababisha hata agizo la serikali la kusomba pamba kutoka AMCOS lisitekelezwe kwa kiwango kikubwa.

Kwamba kampuni za ununuzi hazikuona kwa nini ziingie gharama ya kupeleka magari ya kusomba pamba, wakati wakulima wenyewe wanaipeleka katika viwanda vyao.

Ni vyema kwamba Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Tellack, ameiona dosari hii na akapiga marufuku pamba kununuliwa viwandani, badala ya AMCOS.

Kwa kuwa siku zinazidi kusonga mbele na matayarisho kwa ajili ya msimu ujao yanakaribia, Muungwana ana ushauri kwa serikali kwamba iendeshe operesheni toa pamba kwa wakulima, kama ilifanya kwenye zao la korosho.

Muungwana anashauri hilo ili kuwezesha pamba yote iliyoko kwa wakulima iondoke mikononi mwao kama ilivyoelekezwa na Waziri Mkuu.

Aidha, sambamba na hilo anashauri nguvu ya ziada itumike ili kwamba wakulima ambao tayari wana pamba yao kwenye maghala ya AMCOS, walipwe fedha zao.

Hii ni kwa sababu hadi sasa shughuli ya kuwalipa haki yao hiyo inasuasua pamoja na maagizo ya Waziri Mkuu.

Habari Kubwa