Taifa litastawi tukiimarisha zaidi ulinzi kwa watoto wetu

21Aug 2019
Elizaberth Zaya
Nipashe
Taifa litastawi tukiimarisha zaidi ulinzi kwa watoto wetu

SERIKALI ya Tanzania imeweka sheria, taratibu na miongozo ambayo inashirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhakikisha usalama na ustawi wa watoto nchini.

Lengo la kuweka misingi hiyo ni kuhakikisha mtoto analindwa dhidi ya maovu yote ikiwamo ukatili wa aina zote lakini na kupata haki zake zote.

Hata hivyo, pamoja na kazi kubwa inayofanywa, bado ukatili dhidi ya watoto unaendelea kushamiri na kutupa picha kwamba hitaji la mkakati madhubuti wa kuhakikisha sheria zinazowekwa zinasaidia kupunguza masuala ya ukatili dhidi ya watoto hao kama sio kumaliza kabisa ni la lazima.

Yapo matukio mengi ambayo yamekuwa yakiwakumba watoto wengi yakiwamo ya kubakwa, kulawitiwa na kupigwa.

Na ripoti mbalimbali zinaonyesha kwamba watoto wengi wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo na watu wanaowazunguka.

Wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo katika maeneo tofauti ikiwa ni pamoja na majumbani, wawapo njiani kuelekea shuleni, wanapocheza na wenzao au wanapotembea.

Aidha, kutokana na jamii kutokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu sheria na taratibu za kufuata mara baada ya mtoto kufanyiwa ukatili wa aina yoyote ile, ndiyo sababu mojawapo ambayo inatajwa ya kuviendeleza vitendo hivi vya kuwatesa watoto na kuchangia kuendelea kufanyika.

Suala la utamaduni au desturi na mila ya kuamua kumaliza kimyakimya masuala hayo ya ukatili kwa kisingizio cha kulinda heshima ya mkosaji na hadhi yake katika jamii ni miongoni mwa vyanzo vinavyochangia ongezeko la vitendo hivyo.

Na mbaya zaidi kesi zikipelekwa kwenye mamlaka husika, wenye ushahidi hawafiki mahakamani au mara nyingine mhusika anatoroka na baadaye kesi hufutwa bila kujua hatima ya mtoto aliyepata madhara.

Mpaka sasa kuna idadi kubwa ya watoto waliobakwa na kulawitiwa ambapo takwimu zinaonyesha kwamba mwaka 2015/2016 watoto waliobakwa na kulawitiwa walikuwa 394.

Aidha, mwaka 2016/2017 zilifikia 2,984 huku tafiti zikionyesha kuwa idadi ya watoto waliobakwa itazidi kuongezeka kwa mwaka 2018/2019 na kuwa kubwa zaidi.

Suala hili si la serikali peke yake, ushirikiano unahitajika kutoka kwa jamii yote kwa ujumla ili kushiriki kuutokomeza uhalifu huu ambao unasababisha kuwa na taifa lisilofaa baadaye.

Pia, nguvu za ziada zinahitajika kuhakikisha watoto wanaokumbwa na majanga haya yanasaidiwa kisaikolojia ili kurudi katika hali yao ya kawaida itakayowafanya kuwa viongozi wema na wazazi bora baadaye.

Jamii kwa ujumla inatakiwa iwe macho kupinga vikali ukatili huu unaowakumba watoto wadogo kwa sababu wao ndio taifa la kesho na ndio tegemeo kubwa la taifa katika siku za usoni.

Hivyo hatupaswi kufumbia macho matukio kama haya na kukaa kimya pale tunapogundua mtoto amefanyiwa ukatili, tuchukue hatua ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa katika mamlaka zinazohusika.

Tunatakiwa tufungue macho juu ya haya matukio yanayowakuta watoto wetu na pia tuwe makini na jamii inayotuzunguka kwa ujumla, kwani wengi wao ndio wanaohusika kwa namna moja ama nyingine katika kutekeleza vitendo hivi kwa watoto.

Wazazi kwa sababu ndiyo watu wa kwanza katika maisha ya watoto, wahakikishe wanakuwa karibu na watoto kwa kufuatilia nyendo zao na kuwachunguza.

Walimu na viongozi mbalimbali wa dini wanajitahidi kupiga vita dhidi ya ukatili wa namna hii kwa jamii lakini hali bado ni tete.

Hata hivyo, hawapaswi kukata tamaa, ila kuongeza mwendo na jitihada za kuendeleza vita hivi.

Mamlaka zinazohusika na hatua za kisheria nazo ziendelee kutoa kipaumbele kwa matukio kama haya ili kurahisisha kazi ya kupambana na vita hii na kuokoa viongozi hawa wa siku za usoni.

Jamii ikiwa macho dhidi ya matukio haya na kila mtu akawajibika katika nafasi yake kupambana na vita hii, basi watoto watakuwa salama.