Mkurugenzi kortini madai ya kughushi

21Aug 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mkurugenzi kortini madai ya kughushi

MKURUGENZI Msaidizi wa Maendeleo ya Vijana wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Ester Liwa, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka 22 ikiwamo kughushi, kutumia nyaraka za uongo kwa lengo la kumdanganya-

-mwajiri, ubadhirifu na ufujaji wa zaidi ya Sh. milioni tano.

Alisomewa mashtaka yake katika mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Vick Mwaikomba.

Wakili wa Serikali, Pascal Magabe, alidai kuwa kati ya Machi 11 na Juni 30, 2015 mshtakiwa alitenda makosa hayo katika ofisi za wizara hiyo.

Ilidaiwa kuwa, katika shtaka la kwanza hadi 16, kwa nia ovu mshtakiwa alighushi nyaraka yenye kichwa cha habari ‘Posho ya Kujikimu’ kwa maofisa wa wilaya.

Ilidaiwa kuwa alighushi nyaraka hiyo kwa lengo la kuonyesha watumishi hao walihudhuria mafunzo ya uhamasishaji kwa vijana yaliyofanyika mkoani Singida kati ya Machi 11 - 19, 2015 na kwamba walilipwa Sh. 32,500 kila mmoja wakati akijua si kweli.

Katika shtaka la 17 mpaka 20, mshtakiwa huyo alighushi hati ya malipo ya waandishi wa habari iliyoonyesha Festo Sanga wa Redio Standard Fm, amelipwa jumla ya Sh. 1,030,000 na Emmanuel Michael Sh. 100,000 kama malipo ya kuhudhuria mafunzo hayo.

Liwa pia anadaiwa kughushi hati ya malipo ya jumla ya Sh. 405,000 akionyesha maduka ya vifaa vya ofisi ya Mwaji na Temo, yalilipwa kiasi hicho cha fedha kama gharama ya vifaa vilivyotumika katika mafunzo hayo.

Wakili huyo wa serikali alidai, Juni 25, 2015, akiwa ofisi za Wizara ya Habari, alitumia nyaraka za kughushi akionyesha Sh. 11,177,000 zilitumika katika kipindi cha mafunzo hayo ya vijana mkoani Singida.

Ilidaiwa kuwa kati ya Machi 11 hadi Juni 30, mwaka 2015, mshtakiwa huyo alifanya ubadhirifu na ufujaji wa Sh. 5,425,000, alizokabidhiwa na wizara hiyo kwa lengo la kufanya mafunzo hayo mkoani Singida.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo. Upande wa mashtaka ulidai kutokamilisha upelelezi na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kesi hiyo.

Habari Kubwa