Makonda aona fursa za walimu, biashara SADC

21Aug 2019
Mary Geofrey
Nipashe
Makonda aona fursa za walimu, biashara SADC

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewataka walimu wa lugha ya Kiswahili kuchangamkia fursa ya kwenda kufundisha mataifa mbalimbali duniani na mkoa wake umejipanga kuwasaidia kuifikia fursa hiyo.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Makonda aliyasema jana jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku mbili baada ya Kiswahili kutangazwa kuwa lugha rasmi ya nne ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Awali jumuiya hiyo ilikuwa inatumia lugha tatu za Kiingereza, Kifaransa na Kireno katika shughuli zake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu mkutano wa SADC uliomalizika Jumapili jijini, Makonda alimpongeza Rais John Magufuli kwa kukabidhiwa Uenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Alisema mkoa utashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kuwasaidia walimu waliokosa nafasi za kazi walioko katika jiji hilo kuifikia fursa hiyo muhimu.

"Tutachangamkia hii fursa ya kuhakikisha walimu waliopo kwenye mkoa huu, ambao hawajapata kazi, kwa kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje lakini pia walimu ambao watataka kuanzia mkoani, wanaweza kuanzia kwa Ofisa Elimu Mkoa ili kuchangamkia fursa hii muhimu," Makonda alisema.

Kiongozi huyo wa mkoa pia aliwataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazotokana na uongozi wa Rais Magufuli kipindi chote cha mwaka mmoja kwa kuwa viongozi wa mataifa mbalimbali watakuwa wanakuja nchini.

Alisema ni muhimu wafanyabiashara wa mkoa huo kujipanga kutumia fursa hiyo muhimu kwa ajili ya kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Makonda pia alisema mkoa umepanga kuwa na kampeni endelevu ya kufanya usafi wakati wote katika jiji hilo badala ya kusubiri wakati wa mikutano ya kimataifa.

Habari Kubwa