Shahidi adai kortini wafuasi  Chadema hawakuwa na silaha

21Aug 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Shahidi adai kortini wafuasi  Chadema hawakuwa na silaha

SHAHIDI wa Sita, Koplo Charles, katika kesi ya uchochezi inayowakabili vigogo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwamo Mwenyekiti Taifa, Freeman Mbowe-

-amedai mahakamani kwamba wakati anarekodi picha za video katika mkutano, hakuona wafuasi wa chama hicho wakiwa wameshika silaha ya aina yoyote.

Kadhalika amedai kuwa hakuona wafuasi wa Chadema wakiwashambulia askari polisi wakati akirekodi picha za video katika mkutano wa kufunga kampeni Februari 16, mwaka jana, uliokuwa unafanyika viunga vya Buibui, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Shahidi alitoa madai hayo jana wakati akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya  Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili Kibatala na shahidi:

Wakili: Shahidi Koplo ni cheo cha ngapi katika Jeshi la Polisi?

Shahidi: Cheo cha tatu.

Wakili: Ile video ambayo uliirekodi na mahakama imeiangalia, kuna mahali inaonyesha tarehe ya tukio iliporekodiwa?

Shahidi: Mheshimiwa Hakimu, kielelezo kinajieleza kimerekodiwa lini na wapi.

Wakili: Kielelezo kimeonyesha tukio lilifanyika lini ni sahihi?

Shahidi: Kielelezo kinajieleza washtakiwa walikuwa katika tukio gani na kabla sijaanza kuongoza kuonyesha picha zake. Nilisema mahakamani.

Wakili: Wakati unarekodi picha za video uliwaona wafuasi wa Chadema wakiwa na silaha ya aina yoyote kama vile, mapanga, visu, mawe au marungu?

Shahidi: Sikuwaona wafuasi wa Chadema wakiwa na silaha.

Wakili: Je, uliwaona wafuasi wa Chadema wakiwashambulia askari polisi?

Shahidi: Hapana sikuwaona.

Wakili: Je, ni kweli Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini ajiuzulu au alilazimishwa kama alivyosema Mbowe?

Shahidi: Hapana mimi sifahamu.

Wakili: Kama kweli alijiuzulu kama alivyosema Mbowe, je, kuna kosa gani la jinai?

Shahidi: Ni kosa kulingana na wapi alipozungumzia na mazingira ya mkutano.

Wakili: Kauli ya Mbowe kuhoji Magufuli (Rais Dk.John Magufuli) ni nani ni kosa la jinai?

Shahidi: Mimi sifahamu kwa sababu si mpelelezi wa kesi hii.

Wakili: Una uhakika kama Mbowe anafahamu kama Magufuli ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Shahidi: Mbowe na Watanzania wengine wote tunafahamu Magufuli ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakili: Mbowe alisema Magufuli ni mwepesi kama karatasi kuna tatizo kwa kutoa kauli hiyo?

Shahidi: Mimi kama ofisa wa polisi kauli hiyo niliiona si sahihi katika mazingira yale.

Wakili: Umeshawahi kumpima uzito Magufuli?

Shahidi: Si kazi yangu.

Kesi hiyo inaendelea kusikiliza ushahidi wa Jamhuri leo.

Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi, Dk. Zainabu Mango, Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon na Wakili wa Serikali Jacqueline Nyantori.

Upande wa utetezi uliongozwa na Peter Kibatala, Jeremia Mtobesya, Hekima Mwasipu na Fredy Kiwelo.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya; Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Awali Koplo Charles akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, shahidi alidai kuwa Februari 16, 2018 alipangiwa kazi kama mwandishi wa habari kuandika taarifa kwenye mkutano wa kufunga kampeni wa Chadema katika viwanja vya Buibui.

Alidai kuwa alijiandaa na vitendea kazi vyake ikiwamo kamera ya kupiga picha za video na ilipofika saa 10 alasiri,  alifika katika viwanja hivyo kwa ajili ya kuanza kazi.

Alisema alipofika watu walianza kukusanyika na mshereheshaji alitangaza kwamba viongozi wakuu wa chama wameshafika, baada ya muda wabunge na viongozi wakuu walipanda jukwaani alimsikia Mbowe akitoa kauli za kufanya hamasa ya kuichukia serikali.

"Wanachama walipata hamasa na mihemko iliyosababisha wapate jazba ya kuichukia serikali na vyombo vya ulinzi na usalama, wananchi waliokuwa wamekaa walinyanyuka na kuhamasika, mimi na waandishi wenzangu tulitawanyika pale tuposimama karibu na jukwaa, nilikimbilia kwenye gari polisi kunusuru kamera," alidai Koplo Charles.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka jana, Mbowe na wenzake wakiwa Kinondoni, kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawakuwapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa kuwa siku ya tukio, Bulaya alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Pia ilidaiwa kuwa siku hiyo, katika barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni, Kinondoni, kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa jeshi la polisi, Gerald Ngiichi, na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Ilidaiwa siku ya tukio la kwanza na la pili, katika viwanja vya Buibui, kwenye mkutano wa hadhara, Heche alitoa lugha ya kuchochea chuki alitamka matamshi kwamba "Kesho patachimbika upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii...wizi unaofanywa na serikali ya awamu ya tano... watu wanapotea, watu wanauawa, wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome.”

Maneno hayo yanadaiwa yalikuwa na mwelekeo wa kuleta chuki kati ya serikali na Watanzania.

Washtakiwa wote waliposomewa mashtaka yao kwa nyakati tofauti walikana.

Habari Kubwa