Makonda akomalia matapeli wa ndoa

21Aug 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Makonda akomalia matapeli wa ndoa

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema sakata la wanaume wanaoahidi kuoa wanawake kisha wanawatelekeza, amelihamishia kwenye mjadala wa pamoja ili kupata suluhu ya kudumu ikiwamo kuwafikisha wahusika mahakamani.

Makonda alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, huku akimtaja msanii mmoja maarufu nchini (jina tunalihifadhi), kuwa ni miongoni mwa wanaofanya vitendo hivyo.

Alisema wataanzisha mjadala utakaorushwa mubashara kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili wananchi wapate fursa ya kutoa maoni yao kwa sababu ni tatizo ambalo kwa sehemu kubwa linachochea ongezeko la watoto wa mitaani na mmomonyoko wa maadili.

Alisema amepitia baadhi ya vifungu vya maneno ya Mungu katika Qu’ran tukufu na Biblia takatibu ambavyo vyote vinaeleza kuhusu wanaume au wanawake wanaowalaghai wenzao.

“Mjadala unakuja, tujipange, najua wapo marafiki zangu wengi ambao kimsingi wana ‘promise’ (wanaahidi) kuoa akiwamo (anamtaja msanii huyo), wanaahidi tu kuoa, sasa tujipange inawezekana siku moja wote walioahidiwa kuolewa wakaenda mahakamani,” Makonda alisema.

Alisema suala hilo linaathiri watu wengi zaidi na kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa  ya mwaka 1971 kifungu cha 69, 70 na 71 ni kosa kisheria kuachana na mwanamke uliyeahidi kumuoa na hata zawadi uliyompa mtu wakati wa uhusiano unaweza kwenda kuidai mahakamani.

Alisema suala hilo halifungamani na matakwa ya sheria za dini zinazoruhusu wengine kuoa hadi wanawake wanne, bali ajenda muhimu ipo kwenye kuwapotezea muda wadada ambao pengine wangeweza kuwa na familia zao.

Makonda alisema matokeo ya tabia hiyo iliyokithiri zaidi katika jiji hilo, ni kusababisha ongezeko la watoto wa mitaani, yatima, mmomonyoko wa maadili na ombaomba.

Alisema kama wananchi wataona hakuna haja ya kuingilia suala hilo, hakutakuwa na haja ya kumuhoji kuhusu ongezeko la watoto wa mitaani na mmomonyoko wa maadili kwa sababu kuharibika kwa mahusiano ndio msingi wake.

“Hawakatazwi watu kuoa wake na dini nyingine, zinaruhusu watu kuona wake wengi na hata kama unataka kuona wanawake hata 800 wewe oa, lakini tunachokataza ni kuwapa ahadi wadada wa watu na kuwapotezea muda wao wakati wakijiandaa kuolewa na mwisho wa siku anamuacha akiteseka,” Makonda alisema.

Alisema wanawake wanaofanyiwa vitendo hivyo huishia kuwachukia wanawake, kutokuwa sawa kazini, kuchukua maamuzi ya kuwaumiza, kuathiri utendaji kazi na kuharibu kabisa maisha yao.

Alisema wapo wanaume waliosababisha wanawake watoe mimba, waliowazalisha wanawake, lakini wamewaachia watoto ambao wanalea wenyewe.

“Wapo wengine wanaingia kwenye makubaliano tuzae kabisa, lakini mwisho wa siku ana muacha na mtoto wake na ikitokea baba amekufa aruhusiwi kabisa hata kuaga kwa sababu hatambuliki kwenye ile familia nyingine,” alifafanua zaidi Makonda.

Agosti 12, mwaka huu, Makonda alisema ana mpango wa kuanzisha kanzi data ya ndoa zote zilizopo katika Mkoa wa Dar es Salaam ili kupunguza utapeli wanaofanyiwa wanawake kwa kudanganywa kuolewa.

“Hii ‘data base’(kanzi data) itasaidia mwanamke akiambiwa kuwa anaolewa ataingia katika mtandao na kuangalia jina la mwanaume huyo kama ameoa au la na hata itawasaidia wanawake ambao wameolewa ili kuzuia waume zao wasioe kwa siri. Wanawake mkishaolewa washawishini wanaume waje kusajili vyeti vya ndoa,” alisema.

Habari Kubwa