Chadema yawajibu madiwani wa CCM

22Aug 2019
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Chadema yawajibu madiwani wa CCM

VIONGOZI wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ambalo linaongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamejibu mapigo kuhusu shutuma zinazoelezwa na wapinzani wao, CCM, kwamba kuna mpango-

-wa kutumia mamilioni ya shilingi kwa ajili ya ununuzi wa kompyuta ndogo za mkononi maarufu kama 'Ipad' ili kuwafurahisha madiwani.

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na shutuma hiyo jana, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Michael Kilawila, alisema ununuzi wa ‘Ipad’ hizo hauepukiki.

"Kwanza kwenye kamati tunapitia na kupendekeza na mwisho hoja inakwenda kwenye Baraza la Madiwani ili kupata baraka. Mimi mwenyekiti, sina mamlaka ya kufanya ya kuhamisha fedha yoyote ya halmashauri bila kupitia baraza hilo.

"Wanaolalamika ni wale wanaopenda kujilimbikizia miradi mingi kwenye maeneo yao. Tukienda sasa kwenye uamuzi wa baraza wa kujigeuza kutoka kwenye analogia kwenda kwenye dijitali hakuepukiki,” alisisitiza.

Akionyesha kutofurahishwa na shutuma hizo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Exaud Mamuya, alisema si kweli kwamba wamepanga kutumia Sh. milioni 104 kununua Ipad, bali fedha iliyotengwa kwa ajili ya kompyuta hizo ni Sh. milioni 19.8.

"Hayo malalamiko yao hayana msingi kwa sababu Ipad zitakazonunuliwa ni 66 ambazo zitakuwa ni za waheshimiwa madiwani 46 na wataalamu 20 ambazo kila moja ni Sh.300,000," alisema.

Wiki iliyopita, Madiwani wa CCM, Morice Makoi (Okaoni), Deo Mushi (Kibosho Magharibi), Kamili Mmbando (Kahe Mashariki), Bertin Mkami (Uru Shimbwe) na Anna Lyimo (Kilema Kaskazini), waliamsha zogo hilo kila mmoja akipinga ununuzi huo wa Ipad, badala ya fedha itakayotumika kuelekezwa katika ukarabati wa barabara.

Diwani wa Okaoni (CCM) na Mwenyekiti wa zamani wa halmashauri hiyo, Morice Makoi, alinukuliwa akisema: "Bado miezi 10 madiwani waondoke madarakani, katika halmashauri yetu kuna baadhi ya vyoo vimeanguka, zahanati hazina umeme, leo kuna watu wanachukua milioni 104 wanaamua kwenda kununua Ipad na kununua viti kwa ajili ya ukumbi, wakati viti vipo miaka yote tunakaa."

Habari Kubwa