Wadaiwa sugu TBA watimuliwa

22Aug 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Wadaiwa sugu TBA watimuliwa
  • *Wamo wabunge, watumishi wa umma, taasisi za serikali, zaidi ya bil 1.5/- zinadaiwa…

WAKALA wa Majengo nchini (TBA) imeanza kuwaondoa wadaiwa sugu wakiwamo watumishi wa umma, wabunge na baadhi ya taasisi za serikali wanaodaiwa zaidi ya Sh. bilioni 1.5 kutokana na malimbikizo ya kodi ya muda mrefu.

Wadaiwa hao ni wale wanaoishi kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma, Mtaa wa Area C na D, jijini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Meneja wa TBA, Herman Tanguye, alisema operesheni ya kuwaondoa wadaiwa sugu ni endelevu na imeanzia jijini Dar es Salaam na kuhamia Dodoma kutokana na sehemu hizo kuwa na madeni makubwa kwenye nyumba nyingi ambazo wamewapangisha watu.

Alisema TBA imefikia hatua hiyo baada ya kutoa kwa wapangaji wengine notisi ya siku 30 kwa wapangaji ambao hawajalipa zaidi ya miaka 10 na kuwataka wajiandae kutolewa kwenye nyumba hizo.

"Hili zoezi si kwa Dodoma pekee bali litaendelea nchi nzima ambapo kuna majengo ya TBA," alisema Tanguye.

Alisema kwa mujibu wa mkataba wa nyumba hizo, wanatakiwa kila baada ya mwaka mmoja kulipa, lakini hawajafanya hivyo.

"Unakuta mtu hajalipa kodi ndani ya miaka kumi kinyume na makubaliano ndani ya mkataba aliopangishwa,"alisema.

Kutokana na hilo,  alisema TBA imeamua kuwaondoa wapangaji hao kwa kutumia taratibu stahiki ambazo zinatambulika kisheria na mahakama inatambua.

"Tuliwapa notisi ya siku 30 baadaye tukawaongezea siku 14 wameshindwa kutekeleza ndio maana tumewaondoa," alisema Tanguye.

Naye, Kaimu Meneja Miliki wa TBA, Fredy Mangula, alisema wameshaziondoa familia tatu katika nyumba za eneo la area C na D na operesheni hiyo inaendelea katika nyumba nyingine za eneo hilo.

Alifafanua kuwa uondoaji wa wapangaji hao unafanyika kisheria kwa kushirikiana na kampuni ya Yono Action Mart kutoa vyombo vya wapangaji ambao walishapewa notisi ya kuondoka kutokana na kuwa wadaiwa sugu huku wengine wakimaliza muda wa kuishi maeneo hayo.

"Tunawaondoa wadaiwa sugu kwa kufuata sheria wengi wao walishapewa taarifa ikiwamo notisi na muda wa nyongeza, lakini wamepuuzia agizo hilo," alisema Mangula.

Alisema kinachotakiwa kwa waliopewa notisi za kuondoka, wasibweteke na badala yake watekeleze ndani ya muda waliopewa ili wasije kuondolewa kinguvu na timu inayohusika.

Akitoa ufafanuzi kwa wapangaji wa eneo hilo, alisema wote wanatakiwa kulipa kodi isipokuwa mawaziri ambao wao wanalipiwa kulingana na wadhifa waliokuwa nao.

Alisema, wabunge wanapaswa kulipa kwa wakati ikiwamo kufuata kanuni na taratibu za mkataba wa upangishaji inavyoelekeza.

"TBA tumekuwa wavumilivu sana toka Juni 30 baada ya mwaka wa fedha wa serikali kuisha tuliwapa notisi ikiwamo agizo la utekelezaji wa malipo ya kodi, lakini wengi hawajafanya," alisema Mangula.

Alisema watu wasichukulie mazoea na kuongeza waliopewa agizo wanapaswa kutekeleza.

Alisema lengo ni kukusanya madeni hayo na fedha hizo ni nyingi ambazo zinaweza kufanya kazi ya ujenzi wa nyumba nyingine eneo la Nzuguni ambako kuna hekari 630 kwa ajili ya kujenga nyumba za kupangisha watumishi wanaohamia.

Kwa upande wa wastaafu alisema, wanaondolewa kwa sababu wanaamini tayari wameshakuwa na makazi yao.

"Idadi ya watu wanaohamia makao makuu ni wengi nyumba zilizopo ni chache hivyo ni lazima watu waachie nyumba kama haustahili kukaa," alisema Mangula.

Habari Kubwa