Kagera yakosa umeme na maji kwa siku tatu

22Aug 2019
Lilian Lugakingira
BUKOBA
Nipashe
Kagera yakosa umeme na maji kwa siku tatu

WILAYA tano kati ya saba mkoani  Kagera, jana ziiingia siku ya tatu zikiwa gizani kutokana na kutokuwapo kwa umeme, na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao kwa kutumia umeme.

Wilaya hizo  ni Bukoba, Muleba, Missenyi, Karagwe na Kyerwa, ambazo zinategemea umeme kutoka Uganda.

Katizo la umeme katika wilaya hizo lilianza Jumatatu majira ya asubuhi, huku Ngara na Biharamulo pekee ndizo zinazopata huduma hiyo kutokana na kuwa katika gridi ya Taifa.

Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoa wa Kagera, Mhandisi Shaban Mashaka, alisema tatizo hilo limesababishwa na hitilafu iliyotokea karibu na mji wa Masaka, Uganda.

Mashaka alisema mafundi wa Uganda wanaendelea kushughulikia tatizo hilo, na kuwa Tanesco Kagera imetuma mafundi wake ili washirikiane kutatua tatizo hilo.

Tatizo hilo pia limesababisha kutokuwapo kwa huduma ya maji inayotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa  Mazingira (Buwasa), hali inayosabasha wananchi kuhangaika kutafuta maji ya mito na Ziwa Victoria.

Audax Mutasingwa Mafumbo kutoka Manispaa ya Bukoba, alisema pamoja na kulala gizani kwakukosa umeme, pia amekosa maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

“Namshukuru Mungu leo (jana) mvua imenyesha, nimekinga maji ingawa nimechelewa kwenda kazini, lakini maji kidogo kwa ajili ya matumizi nimepata, ingawa siwezi kufua wala kufanya shughuli nyingine zinazohitaji matumizi makubwa ya maji maana sifahamu kama mvua itanyesha tena,” alisema.

Kagemuro Rweyemamu, mkazi wa Buyekera, alisema kukosa umeme kunawatesa zaidi kinamama, kwa kuwa ndo wanahangaika mtaani kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya familia.

“Hivi unavyoniona nimetoka kuchota maji Bunena kwenye chanzo cha asili ambako ni mbali na makazi yangu, kwa siku ninaweza kuchota ndoo tatu tu kutokana na msururu mrefu na umbali,” alisema.

Mmoja wa wafanyabiashara duka la vifaa vya ofisi, Jasmin Joseph, alisema tangu Jumatatu anafungua ofisi tu, lakini hafanyi shughuli yoyote kutokana na kutokuwa na umeme.

“Hapa nafanya kazi za kutoa kopi, kuchapisha nyaraka, lakini tangu Jumatatu sijafanya kazi yoyote ya kuniingizia kipato, hapa nalipa kodi ina maana nisipofanya biashara ni hasara kubwa kwangu,” alisema Jasmin.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka mpakani mwa Tanzania na Uganda eneo la Mtukula, Kalumuna Richard, anayeishi katika eneo hilo, alisema upande wa Uganda umeme upo ila kwa upande wa Tanzania haupo.

"Hapa Mtukula upande wa Tanzania hatuna umeme, lakini upande wa Uganda wana umeme, hatujafahamu kwa nini maana siyo kawaida," alisema Richard.

Hata hivyo baadhi ya wakazi wa manispaa ya Bukoba wenye mashine za kufua umeme (jenereta) akiwamo aliyefahamika kwa jina moja la Manyati, alisema kwa sasa wanachajisha simu kwa gharama ya Sh. 1,000.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kueleza kuwa liko juu ya uwezo wake, na kuwataka waandishi kuwasiliana na waziri mwenye dhamana.

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alipopigiwa simu jana, hakupokea, na hata alipotumiwa ujumbe mfupi kuombwa ufafanuzi, hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.

Wiki iliyopita, akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Mjaliwa, wakati wa kufungua  maadhimisho ya wiki ya Kagera yaliyolenga kutangaza fursa za uwekezaji, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa,  aliomba serikali kuingiza mkoa huo katika gridi ya Taifa.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), naomba mkoa wa Kagera uingizwe katika gridi ya Taifa ili kuepusha tatizo la umeme kukatika mara kwa mara,” alisema Bashungwai.

Habari Kubwa