Balozi Seif awataka wakazi Kahama kuzaliana kwa wingi

22Aug 2019
Neema Sawaka
KAHAMA
Nipashe
Balozi Seif awataka wakazi Kahama kuzaliana kwa wingi

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amewataka wakazi wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kuzaliana kwa wingi kwa kuwa wana rasilimali za kutosha.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi

Balozi Seif alitoa ushauri huo kutokana na  takwimu za Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama kuzalisha wajawazito 40 hadi 50 kwa siku.

Kutokana na hali hiyo, aliwaomba wananchi hao wasichoke kuzaa ili kuijaza nchi kuenzi utamaduni wao wa kuwa na familia yenye watoto wengi.

Mkoa wa Shinyanga ni mkubwa kijogorafia na kuna maeneo makubwa ya kupata chakula cha kutosha, hivyo wananchi hawanabudi kuendelea kuujaza mkoa wao kwa kuzaliana kwa wingi na kuongeza uzalishaji wa chakula.

Balozi Seif aliyasema hayo alipotembelea Hospitali ya Mji wa Kahama na kuzungumza na wazazi waliojifungua pamoja na wauguzi, huku akisisitiza wauguzi wa hospitali hiyo kuwa la lugha nzuri kwa wagonjwa.

Alisema kitendo cha hospitali ya mji kuwa na idadi ya kuzalisha watoto 40 mpaka 50 kwa siku sio suala la kubeza, na kuongeza kuwa watoto hao baadaye wataongeza nguvu kazi katika kuzalisha chakula ambacho kitakuwa msaada katika familia wanazotoka na mkoa mzima.

Akikabidhi msaada wazazi waliojifungua siku hiyo, mke wa Balozi Seif, Asha Suleiman, aliwataka wazazi kuvitumia vyema vifaa hivyo.

Alisema vifaa alivyotoa ni magodoro, vitanda, mashuka, taulo za kinamama 60, baiskeli za wagonjwa nne, kanga za kwa waliojifungua, maski gloves vikiwa na thamani ya shilingi milioni 3.1.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Tellack, alisema Hopsitali ya Mji wa Kahama ina mahitaji makubwa ya vifaa tiba kwani wagonjwa wengi wanatoka katika halmashauri mbalimbali zilizopo jirani na wilaya kama Geita, Bukombe, Kaliua, Urambo, Nzega na Bongwe kuja kutibiwa.

Habari Kubwa