TBS kufanya ukaguzi wa  kushtukiza nchi nzima

22Aug 2019
Joseph Mwendapole
DAR ES SALAAM
Nipashe
TBS kufanya ukaguzi wa  kushtukiza nchi nzima

BAADA ya kubaini udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wazalishaji wa nondo nchini, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limepanga kufanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye viwanda vyote nchini na kuchukua hatua ya kisheria kwa wazalishaji wasiofuata viwango vya ubora wa nondo.

Shirika hilo lilitangaza uamuzi huo juzi jijini Dar es Salaam kutokana na ukaguzi walioufanya kwenye masoko kubaini kuwapo udanganyifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya wazalishaji wa nondo, jambo ambalo ni la hatari.

Akizungumza baada ya kumaliza kufanyika ukaguzi kwenye maduka yanayouza nondo katika maeneo ya Kawe, Buguruni, Mwenge na Tegeta juzi, Mkaguzi wa TBS, Mhandisi Donard Manyama, alisema katika ukaguzi wao wamebaini kuwapo kwa nondo nyingi zisizokidhi viwango kwenye matumizi ya ujenzi.

"Ukaguzi wetu umebaini kuwapo udanganyifu katika uzalishaji wa nondo kuanzia unene, urefu na madaraja vyote hivyo hakuna ukweli jambo hili ni hatari kama litafumbiwa macho," alisema Manyama.

Alisema kiwango halisi cha urefu wa nondo huwa ni ujazo husiopungua futi 40, lakini zilizopo sokoni baadhi zina futi 39 hadi 34, huku unene yaani ujazo wa kipenyo halisi ni mm 18, lakini zilizopo sokoni nyingi ujazo wake ni tisa hadi sita.

Alizungumzia pia kuhusu udanganyifu unaofanywa na wafanyabiasharara kuuza bei moja kati ya nondo za daraja la BS 300 na 500 kwamba kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Habari Kubwa