Caf yachomoa Yanga kupelekwa machinjoni

22Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Caf yachomoa Yanga kupelekwa machinjoni
  • ***Yabaini pia ujanja wa Township Rollers, yajifua na jua kali la saa tisa alasiri, Zahera asema...

KAMA si Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf), kugomea ombi la Township Rollers la kuhamisha uwanja, Yanga ingeweza kukukutana na dhahama kubwa katika mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa itakayopigwa Jumamosi nchini Botswana, imefahamika.

Township Rollers mapema wiki hii ilituma maombi Caf ikiomba mechi hiyo isichezwe Uwanja wa Taifa, Gaborone na badala yake ikachezwe Uwanja wa University of Botswana (UB), ambao unachukua tariban watazamaji 10,000.

Hata hivyo, Caf iliwakatalia Township Rollers kwa kile ilichoeleza kuchelewa kutuma maombi hayo ya mabadiliko ya uwanja, hivyo ikaelekeza mchezo huo upigwe katika Uwanja wa Taifa, Gaborone ambao ni wa nyasi bandia inapofanya mazoezi Yanga kwa sasa.

Ally Kimrume, Mtazania anayeishi Botswana, aliliambia Nipashe jana kuwa, kama mechi hiyo ingekubaliwa kuchezwa Uwanja wa UB, ingekuwa ni vigumu Yanga kuweza kuchomoza na ushindi hasa ukizingatia ni mdogo halafu ungefurika mashabiki na kuipa presha kubwa timu hiyo ya Tanzania.

"Aise hapa ni kama wametolewa 'machinjoni', sidhani kama pale wangenusurika kipigo maana presha ingekuwa kubwa sana halafu ndipo walipojichimbia wakijifua, lakini hata hivyo hii timu huku ina mashabiki wengi na ndiyo inayojulikana kwa kucheza soka la kiwango cha juu.

"Unaweza kuwa mchezo mgumu kwa Yanga, sema sijui kwa sasa usajili wa timu hiyo ya Tanzania na namna walivyojipanga," alisema Kimrume.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, akizungumza na Nipashe jana, alisema wamefurahi mechi hiyo kupigwa katika Uwanja wa Taifa ambao wenyeji wao wamewapangia kufanya mazoezi hapo.

"Waliomba mechi kupelekwa Uwanja wa UB, lakini Caf imewakatalia kwa sababu walichelewa kupeleka maombi yao, hivyo mechi yetu itachezwa hapa tunapofanya mazoezi kama ilivyopangwa awali," alisema Mwakalebela.

Alisema Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera amependekeza wachezaji kufanya mazoezi saa tisa mchana lengo likiwa ni kuzoea mazingira ya jua kali kutokana na aina ya uwanja wa nyasi bandia watakaoutumia katika mchezo huo.

 “Wote tunafahamu mazingira ya uwanja wa nyasi bandia, siku zote unashika joto kwa sababu ya jua kali linalopiga uwanjani hapo, hivyo benchi la ufundi kwa kushirikiana na viongozi tumeshauriana kufanya mazoezi saa tisa alasiri," alisema.

Yanga inahitaji sare ya kuanzia mabao mawili ama ushindi ili kusonga mbele kufuatia mechi ya awali Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kumalizika kwa sare ya bao 1-1

Timu itakayoibuka na ushindi itakutana na mshindi wa mechi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia katika raundi inayofuata.

Habari Kubwa