Kabudi akiri upinzani Kiswahili SADC

22Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kabudi akiri upinzani Kiswahili SADC

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Tanzania ilipata upinzani mkubwa katika jitihada zake kuishawishi Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kukifanya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha nne rasmi za shughuli za jumuiya hiyo.

Prof. Palamagamba Kabudi

Mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi za SADC uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, ulikipitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne ya shughuli zake. Awali jumuiya hiyo ilikuwa inatumia Kiingereza, Kifaransa na Kireno.

Hata hivyo, katika mkutano wake na wahariri na waandishi wa habari jijini jana, Prof. Kabudi alisema haikuwa rahisi kwa Tanzania kuishawishi jumuiya hiyo iridhie Kiswahili kutumika katika shughuli zake.

"Tumepata upinzani mkubwa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne kwenye mikutano na shughuli za SADC. Baadhi ya mataifa yalipinga kwa hoja kwamba ni lugha ya kabila fulani na hatuwezi kuwalaumu," Prof. Kabudi alisema.

Waziri huyo aliwataka Watanzania kutobweteka badala yake watumie fursa hiyo kujipatia ajira.

"Wataalamu wengi wanaofundisha Kiswahili Amerika na Ulaya kwa sasa wanatoka Kenya na Congo. Tuchangamkie fursa hii muhimu, lakini lazima tujifunze lugha nyingine za kigeni hasa Kifaransa na Kireno.

"Mshindani wa Tanzania katika fursa hii ya Kiswahili kusini mwa Afrika ni Congo. Lazima niuseme ukweli huu maana maeneo mengi Congo ni wazungumzaji wakubwa wa Kiswahili na wanaijua vizuri lugha ya Kifaransa," alisema.

Prof. Kabudi pia alisema Tanzania ambayo imepewa uenyekiti wa SADC kwa mwaka mmoja hadi Agosti mwakani, inaunga mkono maombi ya Burundi kujiunga na jumuiya hiyo, akibainisha kuwa nchi hiyo imefuzu vigezo kwa zaidi ya asilimia 70.

"Kuna maeneo mawili ambayo Burundi inapaswa kuyafanyia kazi. Mojawapo ni kuihakikisha jumuiya kwamba itakuwa na uwezo wa kulipa ada ya mwaka ya mwanachama wa SADC," alisema.

Prof. Kabudi ambaye ni mwalimu wa sheria, akifundisha kwa muda mrefu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), pia alisema Tanzania itasimamia kidete uondoaji wa vikwazo dhidi ya Zimbabwe ili kuinua uchumi wa nchi hiyo tajiri wa madini.

Katika mkutano wake huo na wanahabari, Prof. Kabudi alivipongeza vyombo vya habari kwa kazi kubwa viliyoifanya katika Mkutano wa 39 wa SADC.

"Kwa kweli vyombo vya habari vimetekeleza wajibu wake vizuri sana katika mkutano huu. Waliokuwa na shaka na uongozi wa Tanzania katika eneo hili la SADC, vyombo vya habari vimewafanya sasa waamini Tanzania inaweza.

"Vyombo vya habari vilishikamana na serikali katika kipindi chote cha shughuli za SADC. Mkutano umemalizika lakini shughuli ndiyo kwanza zinaanza. Kutakuwa na mikutano zaidi ya 30 ya kisekta itakayofanyika hapa Tanzania.

"Mikutano inalenga kuwa na viwanda endelevu kwa lengo la kuongeza ajira na uzalishaji wa bidhaa bora," Prof. Kabudi alisema.

Waziri huyo aliongeza kuwa wakati wa vikao hivyo vya kisekta, watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa uondoaji vikwazo vya kibiashara miongoni mwa nchi za SADC ili kuinua uchumi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Habari Kubwa