Shein apigia debe matumizi Kiswahili

24Aug 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Shein apigia debe matumizi Kiswahili

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Muhamed Shein, amevitaka vyombo vya habari nchini kutumia vyema lugha ya Kiswahili katika utangazaji na uandishi wa habari.

Akipokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi kwa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kwa kipindi cha Julai, 2018 hadi  Juni, mwaka huu jana, Dk. Shein aliitaka wizara kukutana na wahariri wa vyombo vya habari kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo.

Dk. Shein alisema Zanzibar ndiyo kitovu cha lugha fasaha ya Kiswahili, hivyo ni vyema kuitumia kwa ufasaha.

Aliitaka idara ya Habari (Maelezo) Zanzibar kuweka utaratibu mzuri wa kutoa vibali vya kupiga picha na kuhakikisha sheria za nchi zinafuatwa hasa kwa wageni wanaofika Zanzibar kufanya shughuli hizo.

Pia alisisitiza haja ya kuendelea kuzitunza na kuzihifadhi vyema nyaraka za serikali.

Kuhusu uendeshaji wa shughuli za makumbusho, Dk. Shein aliitaka idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale, kuendelea kuhamasisha jamii ya Wazanzibari, wakiwamo wanafunzi, kutembelea maeneo hayo ili kufahamu historia ya asili ya Zanzibar.

Aidha, alisema iko haja ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano mwema uliopo katika sekta ya utalii, kati ya Zanzibar na Indonesia kwa kushirikiana na Chuo cha Utalii cha Bali cha nchini humo.

Dk. Shein aliupongeza uongozi wa wizara kwa kutekeleza vyema majukumu ya kazi zake sambamba na kuandaa kwa umakini mkubwa taarifa za utekelezaji wa mpango kazi.

Naye Waziri wa Wizara hiyo, Mahamoud Thabit Kombo, alisema katika kipindi cha Julai, mwaka jana hadi Juni, mwaka huu, wizara imetekeleza miradi mikuu mitatu, ukiwemo ujenzi wa studio na ofisi za ZBC Pemba kupitia Kampuni ya ujenzi ya Chuo cha Mafunzo Zanzibar. Alisema awamu ya kwanza ya kazi hiyo inayohusisha ghorofa ya chini imekamilika.

Alisema katika awamu ya pili ya ujenzi huo, mkandarasi ataendelea na ujenzi wa ghorofa ya pili, uezekaji, upigaji wa plasta  na kupaka rangi.

Pia alisema katika kipindi hicho, wizara ilishughulikia mradi wa kuimarisha maeneo ya kihistoria ya Fukuchani na Makamandume, mradi uliogharimu Sh. milioni 850.

Alisema Wizara imelifanyia matengenezo makubwa eneo la kihistoria la Fukuchani, ili kurudisha sura na haiba yake ya awali pamoja na matengenezo  eneo la kihistoria la Mkamandume yanaendeleo.

Waziri alisema matengenezo hayo yanaenga kuziimarisha kuta za asili katika pande tatu za jengo hilo na kuvirudisha baadhi ya vivutio vya asili vilivyomo ndani ya eneo hilo.

Vilevile alisema katika kipindi hicho wizara ilishughulikia mradi wa kuimarisha utalii kwa wote, ukihusisha ujenzi wa kituo cha utalii katika eneo la Kwa Bihole Bungi, mradi utakaotumia Sh. Bilioni 1.3 hadi kukamilika kwake.