Watakiwa kujihadhari tishio la mamba

24Aug 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Watakiwa kujihadhari tishio la mamba

SERIKALI ya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, imewataka wananchi wa Shehia za Mchikichini na Hawaii kuchukua tahadhari maalumu kufanya shughuli za kijamii katika Mto Barafu.

Tahadhari hiyo imetolewa baada ya kubainika kuwapo kwa mamba huku serikali ikichukua hatua za haraka kuondosha kadhia hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema hayo jana baada ya kufanya ziara maalum katika maeneo hayo kwa kukamatwa kwa mamba katika mto hua ambao wameanza kuzua taharuki kwa wananchi wa shehia hizo.

Akizungumza na wananchi, viongozi wa wilaya ya Magharibi A, Ayoub alisema kwa sasa serikali ya wilaya, shehia na wataalamu wa idara ya misitu watafanya kazi kwa pamoja kuondoa tatizo hilo mara moja na kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao kwa usalama.

Mamba hao waliobainika katika Mto Barafu, inasemekana wanatoka katika kituo cha Zanzibar Park baada ya uongozi wa kituo hicho kukiri  kuharibika kwa miondombinu wanamofugiwa wanyama hao na pengine baadhi ya mayai kusambazwa na maji yanayopita katika eneo la hifadhi hiyo na kuelekea maeneo ya Mchikichini ambako inakisiwa ni kilomita tatu kutoka katika hifadhi hiyo.

Naye Ali Mwinyi, mtaalam kutoka idara ya Misitu, amekiri kupokea na kuhifadhi baadhi ya mamba waliokamatwa katika eneo hilo na kuwatoa hofu wananchi kuwa  bado ni wadogo na hawawezi kuwa na madhara kwa binadamu.

Imebainika kuwa mamba wanne wamepatikana katika eneo la Mto Barafu na kikundi cha vijana 12 ambao wanawakamata mamba hao huku serikali za wilaya na mkoa zikiahidi kuanza kusafisha eneo lote la mto kuanzia kesho kwa kushirikiana na uongozi wa Zanzibar Park, wananchi na wataalamu wa idara ya misitu.

 

 

 

Habari Kubwa