Kigogo CCM atamani kurejea kufundisha

24Aug 2019
Gwamaka Alipipi
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kigogo CCM atamani kurejea kufundisha

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema siku moja atarudi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuendelea na kazi ya kukuza maarifa.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally.

Aliyasema hayo juzi wakati akizindua mradi wa kuwasha taa za barabarani Mtaa wa Chief Kunambi. Taa hizo zinatumia nishati ya jua.

"Hata mimi niliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu wakati nikiwa chuoni hapa, lakini kwa sasa nipo kwenye siasa, nipo likizo na kila siku nafikiria kurudi hapa kufundisha.

"Mungu akinijalia ipo siku nitarudi hapa kuendelea na kazi ya kukuza maarifa," Dk. Bashiru alisema.

Alieleza kuwa anakikumbuka chuo hicho katika maisha yake, akikumbusha kuwa mwaka 1997 alipokuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni hapo, kulikuwa na uhaba mkubwa wa makazi ya wanafunzi.

Alisema kipindi hicho waliunda cheo cha ‘cumpus’ ambacho hakikuwapo na lengo kuu lilikuwa ni kuanzisha harakati  za ujenzi wa mabweni ya wanafunzi na yeye kuwa Rais.

Alisema harakati hizo zilizaa matunda na kufanikisha kujengwa kwa mabweni ya wanafunzi katika eneo la Mabibo jijini.

Dk. Bashiru aliutaka uongozi wa UDSM wakati wakisherehekea kumbukizi ya kuanzishwa kwa chuo hicho Oktoba 25, mwaka huu, waendeshe pia matukio ya kitaaluma ya kuunga mkono juhudi za viongozi wa Jumuiya ya Nchi Kusini mwa Afrika (SADC) za kuhakikisha Zimbabwe inaondolewa vikwazo.

"Oktoba 25, mwaka huu, ninajua ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa UDSM, tarehe hiyo pia imepangwa na wakuu wa SADC iwe ni siku ya kutoa tamko kwa mataifa ya Ulaya kuiondolea vikwanzo Zimbabwe, niwaombe na nyie mshiriki katika mpango huo, siyo kwa kupiga kelele, bali kwa kuendesha matukio ya kitaaluma," Dk. Bashiru alishauri.

Kigogo huyo wa CCM pia aliwataka wenyeviti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere kutenda haki kwa kukuza maarifa kupitia jina la Mwalimu Nyerere.

Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. William Anangisye, alisema mradi huo wa taa umegharimu Dola za Marekani 49,300 (Sh. milioni 113) ukitekelezwa na Kampuni ya Stecko iliyosimika nguzo 36 za taa.

Alisema taa hizo zina uwezo wa kufanya kazi kwa saa 50,000 bila ya kubadilishwa na zilianza kuwekwa Juni hadi Julai mwaka huu.

"Taa hizi ni za kisasa, zinajiwasha na kujizima zenyewe ifikapo asubuhi, mradi huu ulikuwa ni wazo la Dk. Bashiru ambalo Ubalozi wa China ulilifadhili," Prof. Anangisye alisema.

Aliongeza kuwa kujengwa kwa taa hizo kutaimarisha ulinzi na usalama katika mtaa huo na zitapunguza gharama za umeme kwa kuwa pesa zilizokuwa zinatumika kulipa Shirika la Umeme (Tanesco), sasa zitatumika kwa mambo mengine muhimu.

Balozi wa China nchini, Wang Ke alisema: "Tulipokea ombi la kujenga taa kutoka kwa Dk. Bashiru Ally na Prof. William Anangisye, nilipotembelea ni kweli nikaona kuna giza, nikaona kuna umuhimu wa kuweka taa."

Habari Kubwa