Vigogo halmashauri watimuliwa bungeni

24Aug 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Vigogo halmashauri watimuliwa bungeni

OFISI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) imeagizwa kufanya ukaguzi maalum wa upotevu wa zaidi ya Sh. bilioni tatu ndani ya miezi mitatu katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyangh'wale mkoani Geita.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Abdallah Chikota

Agizo hilo lilitolewa juzi na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Abdallah Chikota, baada ya kufanya mahojiano na viongozi wa halmashauri hiyo kuhusu hoja za ukaguzi za CAG kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Alisema waliamua kuwatimua vigogo wa halmashauri hiyo kutokana na kushindwa kujibu hoja zilizoibuliwa na CAG na kwa kiasi kikubwa ripoti waliyopelekewa na ofisi ya CAG imejaa ubadhirifu.

Chikota alisema pamoja na kwamba kuna watumishi ambao wapo ndani na wengine kesi zao ziko mahakamani, bado kuna wengine wako nje, hivyo kuna haja CAG afanye ukaguzi huo maalum.

"Wengine wapo nje kwa sababu hawakufanyiwa ukaguzi ili nao wajumuishwe na kuchukuliwa hatua," Chikota alisema.

Alibainisha kuwa kati ya fedha hizo, kuna vitabu 50 vya vyanzo taarifa zake hazikuwasilishwa.

"Kuna hati za malipo zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni moja hazikuwasilishwa, kuna uhamisho wa fedha bila kuonyesha shughuli zilizofanyiwa kiasi cha Sh. bilioni 1.7, malipo yasiyo na viambatanisho Sh. milioni 339.7," alisema.

Chikota pia alieleza kuwa Sh. milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya hazionekani na kituo hakijajengwa huku akisisitiza halmashauri hiyo imekuwa na changamoto ya kuchelewa kukamilisha miradi ya maendeleo.

"Kuna fedha za P4R kwa shule za sekondari kiasi cha Sh. milioni 576 zimetumika nje ya malengo yaliyokusudiwa, fedha kwa ajili ya mradi wa maji wa Sh. milioni 74.1 ambazo taarifa ya benki inaonyesha Sh. milioni 71.1 hazipo," alisema.

Aliongeza kuwa kwa kiasi kikubwa halmashauri hiyo haiwatendei haki wananchi wake maana fedha zilizoibwa ni za miradi ya maendeleo.

Alisisitiza kuwa watendaji hao wamekiuka maadili ya utumishi wa umma na kuamua kuzitafuna fedha hizo ambazo kati yake, Sh. bilioni 1.9 ni za miradi, Sh. milioni 700 zimefanyiwa kazi huku Sh. bilioni 7.2 zikiwa zimeteketezwa.

"Kuna fedha kwa ajili ya mradi wa maji Sh. milioni 400 hazipo na hazijawasilishwa kwa mkaguzi, hivyo kamati imeamua tusiwahoji, tumemwagiza CAG wa kanda hiyo akafanye kazi ya ukaguzi maalum ndani ya miezi mitatu alete majibu," alisema.

Alisisitiza lazima ukaguzi ufanyike na wahojiwe kutokana na fedha kutumika bila kufuata utaratibu.

"Hatuwezi kufumbia macho suala hili maana hata kama kuna watendaji wapya kwa sasa, hatuwezi kuwasifia wakati wizi bado unaendelea kufanyika," alisema.

Chikota pia aliagiza Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kufanya maboresho ya kitengo cha kufuatilia fedha ili kuepuka ubadhirifu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais - Tamisemi, Mwita Waitara, aliahidi kuyafanyia kazi mapendekezo ya kamati hiyo na baada ya uchunguzi kukamilika, hatua kali zitachukuliwa na hakuna atakayesalimika hata kama amestaafu.

Alisema haiwezekani kufumbia macho wakati wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali huku wakitegemea miradi hiyo itatue changamoto zao.

"Mradi hakuna kisa mtendaji mmoja aliyeaminiwa kushindwa kufanya kazi, viongozi wa halmashauri hii mnapaswa kutambua kuwa uamuzi huu wa kamati si mzuri kwetu,"alisema.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Denis Bandisa, aliihakikishia kamati kuwa watayafanyia kazi kwa kuipa ushirikiano ofisi ya CAG itakapokuwa ikifanya ukaguzi huo.