Mawakili 14 serikali wamkabili Lissu

24Aug 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mawakili 14 serikali wamkabili Lissu

JOPO la Mawakili 14 wa Serikali wakiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Clement Mashamba, wamewasilisha hoja nane za kupinga maombi ya Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kwamba hayana mashiko kisheria kwa kuwa aliyemwakilisha kuyafungua hana mamlaka kufanya hivyo.

Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.

Jopo hilo kwa nyakati tofauti limeomba maombi hayo yatupiliwe mbali na mlalamikaji alipe gharama za kesi dhidi ya walalamikiwa ambao ni  Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Pingamizi hilo lilisikilizwa jana katika Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam chini ya Jaji Sirilius Matupa.

Dk. Mashamba alidai kuwa walalamikiwa wamewasilisha pingamizi lenye sababu nane kupinga maombi yaliyowasilishwa na Lissu kupitia mawakili wake, Peter Kibatala, John Mallya na Jeremiah Mtobesya.

Alidai kuwa katika sababu hizo nane, ndani yake kwa ujumla kuna hoja nne ambazo kwa nyakati tofauti zitawasilishwa na mawakili wenzake wa serikali na pale inapohitajika atasaidia.

Alizitaja hoja hizo nne kuwa ni kuhoji kwanza, mamlaka ya mahakama kusikiliza maombi kama yalivyowasilishwa, pili, kama mleta maombi ana uwezo wa kufanya hivyo, tatu kama maombi hayo yaliwasilishwa katika mahakama yenye mamlaka na nne, kama nafuu zilizoombwa ni sahihi kutolewa na mahakama hiyo.

Akianza kuwasilisha hoja, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abubakar Mrisha, alidai maombi yaliyowasilishwa mahakamani hayana nguvu kisheria kwa sababu maombi au mashauri yanapofikishwa mahakamani lazima yawe yamezingatia vigezo sita.

Mrisha alidai kuwa kigezo cha kwanza kama maombi yaliletwa ndani ya miezi sita baada ya jambo husika kutolewa uamuzi, pili, mwombaji awe anaelewa vizuri shauri, uamuzi uwapo kisheria, iwe hakuna namna nyingine ya kufanya kuhusu uamuzi huo, kama mahakama itasikiliza na kuona kuna haja ya kutoa uamuzi na sita, maombi yanatakiwa yawe katika nia njema na wala si kwa kupotosha au kuwa na lengo la kujinufaisha.

" Mtukufu Jaji, maombi yaliyopo mbele yako yametimiza kigezo kimoja ambacho ni kuyawasilisha maombi ndani ya miezi sita. Ukitazama vigezo vitano vimekosekana, hakuna uamuzi wowote ulioambatanishwa katika maombi ili mahakama iyapitie na kuyatolea uamuzi. Maombi yoyote ni muhimu kisheria kuambatanisha uamuzi  unaomkumba," alidai Mrisha.

Akifafanua hoja za pingamizi hilo, alidai kuwa kiapo cha Alute alichoambatanisha ni nakala ya magazeti na si uamuzi, hivyo hakuna uamuzi wowote uliotolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, isipokuwa alitimiza matakwa ya kisheria kwa kumwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa kwamba kuna kiti kiko wazi.

Wakili wa Serikali Mkuu, Lucas Marunde, alidai waleta maombi wanaomba mahakama imlazimishe Spika alete tamko lake la kumvua ubunge Lissu mahakamani na wadai wapewe nakala.

"Mheshimiwa Jaji, Sheria ya Uchaguzi Na. 37(3) Sura ya 343 ya mwaka 2015 inasema Mbunge anapokuwa hayupo katika kiti chake kwa mikutano mitatu mfululizo ya Bunge bila kutoa taarifa kwa Spika anamfahamisha Mwemyekiti wa Tume ya Uchaguzi kwamba kiti kiko wazi," alidai.

Alidai si Spika anayetoa tamko bali anatoa taarifa na hajishuhulishi na kitu kingine chochote na kwamba katika kesi hiyo mwombaji hakuwepo katika kiti chake cha ubunge.

Wakili Marunde alidai hakuna uamuzi wowote kutoka kwa Spika, hivyo wanaomba maombi yatupwe kwa gharama.

Hoja zingine ziliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu George Mundepo, ambaye alidai kwamba mleta maombi, Alute Mughwai, hana sifa ya kufungua maombi kwa niaba ya Lissu.

Alidai sheria inaruhusu madai kufunguliwa na mhusika au anayemwakilisha mwenye mamlaka kisheria lakini shauri lililopo limewasilishwa na Tundu Lissu kupitia mwakilishi wake, Mughwai.

Kutoka na hoja hizo, aliomba mahakama iyatupe maombi kwa kuwa pamoja na mambo mengine, aliyeyawasilisha hana sifa ya kufanya hivyo.

Jaji Matupa jana alitakiwa kusikiliza maombi ya zuio la muda la kuapishwa kwa Mbunge Mteule wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, na maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge wa Lissu lakini haikuwezekana baada ya Jamhuri kuwasilisha pingamizi la awali.

Maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge yalifunguliwa na Lissu kupitia mawakili wake chini ya hati ya dharura, kupitia kaka yake, Wakili Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa ombi namba 18 la mwaka 2019, Lissu anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili mahakama hiyo itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe (Lissu) taarifa yake ya kumvua ubunge.

Anaiomba mahakama hiyo itengue na kutupilia mbali uamuzi huo wa Spika Ndugai kumvua ubunge.

Mwombaji huyo anaomba mahakama itoe amri ya kusimamisha kuapishwa kwa  Mtaturu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika hati ya dharura, Lissu anaiomba mahakama hiyo isikilize na kutoa uamuzi wa maombi yake haraka kuwa vinginevyo Mtaturu ambaye Julai 19, mwaka huu, alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, ataapishwa kushika wadhifa huo, anadai atakuwa ameathirika kwa kuwa atapoteza haki zake zote, kinga na maslahi yote yanayoambatana na wadhifa wake wa ubunge.

Uamuzi wa kumvua ubunge ulitangazwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Juni 28, mwaka huu wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, huku akitaja sababu mbili.

Spika Ndugai alizitaja sababu hizo kuwa ni kushindwa kuhudhuria vikao vya bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha kwa maandishi mahali aliko na pili ni kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Hata hivyo, Ndugai alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni Katiba ya nchi.

Habari Kubwa