Hongera Yanga, Azam, lengo liwe kulinda nafasi kwanza

26Aug 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hongera Yanga, Azam, lengo liwe kulinda nafasi kwanza

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, Yanga na Azam FC zimefanikiwa kutinga hatua za raundi ya kwanza kwenye michuano hiyo.

Yanga imefanikiwa kutinga hatua ya Ligi ya Mabingwa kwa kuitoa Township Rollers kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoka sare nyumbani na kushinda ugenini bao 1-0.

Azam yenyewe imetinga raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuisukumiza nje Fasil Kenema ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 3-2, ikifungwa bao 1-0 ugenini na kushinda mabao 3-1 nyumbani.

Huu ni mwanzo mzuri kwa timu za Tanzania ambazo ni mara ya kwanza kuwa na idadi ya timu nne kwenye michuano ya kimataifa.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf), liliipa Tanzania nafasi nne badala ya mbili, hii ikichagizwa na Simba kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.

Kwa kuanzia angalau timu mbili zimeshafanikiwa kutinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo na hii imekuwa ni faraja kwani kama timu za Tanzania zingetolewa ingekuwa ni kilio kikubwa.

Nasema kilio kwa sababu pamoja na kwamba Tanzania imeingiza timu nne, lakini haina pointi nyingi, hivyo inaweza kuengulia mwakani kuingiza idadi hiyo kama klabu hizo zikifanya vibaya.

Nyuma ya Tanzania kuna nchi kama Kenya na nyingine ambazo zinaifukuza nafasi hiyo, na kama klabu zao zikifanikiwa kufanya vema na sisi kufanya vibaya, tunaweza kuzidiwa pointi na mwakani kujikuta tukirudi kwenye idadi ya timu zilezile mbili.

Kuna baadhi ya nchi Afrika kama Misri, Congo DR, Algeria, Tunisia na nyingine timu za klabu zimekuwa zikifanya vema karibuni kila mwaka tangu zamani, hivyo hizi zina pointi nyingi mno na hata kama timu zao zote nne zitatolewa kwenye michuano kwa miaka mitatu, bado zitaendelea kupeleka wawakilishi wanne.

Tanzania ni moja kati ya timu ambazo ndizo za chini, zikiwa na pointi chache, hivyo kinachotakiwa ni klabu zetu kujituma na kujitahidi kusonga mbele ili kujazia pointi ambazo zitafanya nafasi ya timu nne kuendelea kuwa salama.

Nitoe pongeza kwa Yanga ambayo pamoja na matatizo kadhaa, kutofanya vema nyumbani na kuchukuliwa kuwa ndiyo kama vile imetoka, lakini ilipigana kufa kupona ugenini na kufanikiwa kusonga mbele, kuihakikishia Tanzania kuwa imo bado kwenye michuano hiyo.

Azam nayo baada ya miaka michache na kusuasusa imeonekana imerudi kivingine, nayo kwa jinsi ilivyo, pamoja na matunzo inayoyapata ina wajibu wa kufanya vema ili kuhakikisha mwakani Tanzania inapeleka tena timu nne.

Tukubaliane kuwa kutwaa Kombe la Afrika, au Kombe la Shirikisho kwa timu hizi si kazi rahisi, lakini sasa malengo yao yawe ni kutinga hatua ya makundi tu.

Lengo la hatua hiyo, si tu kuzifanya timu hizo kujiingizia kitita cha pesa kutoka Caf, lakini pia kuikusanyia nchi pointi ili mwakani Tanzania ipeleke kwa mara nyingine tena timu nne, lakini pia kuzifanya hata zile nchi ambazo zinatukaribia kuziacha kwa mbali.

Tanzania ikishakuwa na uhakika wa kuwa inaingiza timu nne karibuni kila mwaka ni faida kubwa kwani hata Ligi Kuu ya Tanzania inakuwa na ushindani, kwa kuwa timu hazigombei tu kuwa bingwa, lakini pia zinagombea nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye mechi za kimataifa.

Kwa hali hiyo kutakuwa hakuna timu inayokubali kufungwa kizembezembe, kwani kila moja itakuwa ikitafuta kuwamo kwenye nafasi nne za juu. Pamoja na pongezi, nitoe pia angalizo kuwa mechi za raundi ya kwanza hazitokuwa rahisi kama hizi.

Kwenye michuano hii kila raundi timu inayoingia inakuwa ngumu kuliko ya kwanza. Kwa maana hiyo timu za Yanga na Azam zisibweteke na badala yake zianze maandalizi ya mechi zinazofuata za raundi ya kwanza mwezi ujao.

Habari Kubwa