‘Waacheni wakimbizi warudi nyumbani’

27Aug 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
‘Waacheni wakimbizi warudi nyumbani’

KILA la kheri Tanzania na Burundi kwa kuafikiana kurejesha wakimbizi 2,000 kila wiki nchini kwao kuanzia Oktoba mwaka huu, jambo ambalo litawarudisha  nyumbani maelfu ya wakimbizi ambao pamoja na kutengwa na familia zao wanapata  wasaa mwingine wa kuungana na kujenga taifa lao.

Hatua ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao inakuja baada ya kujiridhisha kuwa kuna amani na utulivu nchini Burundi na raia wanastahili kurejea makwao hatua inayotangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola kwa upande wa Tanzania na Paschal Barandagiye wa Burundi.

Tangazo hilo kama lilivyoelezwa linawahusu wakimbizi waliokuwa wanaishi kwenye makambi ya Nduta na Mtendeli mkoani Kigoma.

Ni jambo la mafanikio katika kulinda maisha na uhuru wa asili wa raia wa Burundi ambao walizaliwa huru na wanatakiwa kupata haki hiyo hadi mwisho wa maisha   na si kuishi ugenini.

Kuwa mkimbizi ni jambo lisilotabirika na pengine hata kukwepeka kutokana na mivutano ya kisiasa iliyoko duniani leo.

Hata hivyo, jumuiya za ushirikiano za kanda mbalimbali Afrika kama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya Maendeleo ya Uchumi ya  Kusini mwa Afrika (SADC) moja ya majukumu yake ni kuwa na sera na taratibu zinazolinda amani na utulivu miongoni mwa mataifa wanachama ili kuepusha vita na wakimbizi.    

Vurumai za kisiasa ni mambo yanayowanyima raia uhuru wa asili wa kuishi katika mataifa waliyozaliwa na kuendesha maisha yao.

Hivyo ni vyema Burundi ikapigania uwapo wa haki na usawa ili kuondoa vita katika nchi yake na kuwapa raia wake haki ya kuwa huru ndani ya ardhi yao.

Burundi imejinasibu kuwa iko salama na raia wake walioko Tanzania wanaweza kurudi nyumbani, lakini yakatolewa maelezo na wakimbizi hao kuwa wanatishiwa na mashiriki ya kuhudumia wakimbizi kuwa Burundi hakuna amani ili wafanyakazi hao waendelee kuishi na wakimbizi hao makambini.

Licha ya kwamba Waziri Lugola ameagiza ufanywe uchunguzi ili kuwafahamu wanaowaongopea wakimbizi ukweli ni kwamba, Waswahili wanasema hakuna lisilo na mwisho au marefu yasiyo na ncha.

Wakimbizi hawawezi kuishi kambini muda wote  au maisha yao yote, kisa kuna maofisa wanaowatishia kuwa nyumbani kwao hakuna amani. Hata hao maofisa nao watafakari mienendo yao kwa kuwa ukimbizi ni kama ‘utumwa’.

Ukimbizi una athari kisaikolojia, kiuchumi, kihisia na wakati mwingine ni kama kukwama kimaisha kutokana na changamoto kama hizo za ukosefu wa amani nyumbani.

 Wakimbizi wengi wanakumbuka nyumbani pamoja na wale waliobaki huko nyumbani hawa ni wana familia kuanzia wazazi, dada na kaka, wenza na watoto. Lakini pia kuna kile walichokiacha iwe mali, malengo na hata kazi zilizofanyika zikiwamo hati za ardhi, vyeti vya kitaaluma na mambo mengi ambayo kabla ya kuwa mkimbizi mtu aliyafanya.

Chondechonde waacheni wakimbizi warudi nyumbani, msiwarubuni kwa lolote wapeni nafasi ya kuungana tena na familia zao, kuziona tena kazi walizozifanya na kutimiza ndoto zao kabla hawajawa katika hali ya kukimbia nchi zao.

Itoshe tu kusema kuwa wakimbizi nao ni watu waliozaliwa huru wanaohitaji kuwa huru na kufurahia maisha yao. Waacheni warudi Burundi msiwazuilie kwa lolote kwa kuwa uraia wao ni haki yao ya kuzaliwa, lakini ardhi yao ni zawadi waliyopewa na Mungu alipoumba ulimwengu na kutawanya mataifa.

Kila la heri wakimbizi wanaorudi nyumbani tunawatakia mafanikio na fanaka zote kila wanapoanza tena maisha yao ndani ya ardhi  waliyopewa wakati wa kuumbwa ulimwengu.

Habari Kubwa