Wanufaika mikopo elimu ya juu walipe walichokopeshwa

27Aug 2019
Raphael Kibiriti
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wanufaika mikopo elimu ya juu walipe walichokopeshwa

GAZETI hili limekuwa na habari kubwa katika ukurasa wake wa mbele kwa nyakati tofauti mwezi huu, zilizoandikwa zikieleza kwa kina namna mikopo ya elimu ya juu ilivyogeuka shubiri kwa wanufaika.

Mikopo ambayo inatolewa na serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi  wa Elimu ya Juu (HESLB), kwa lengo la kuwezesha wanafunzi wenye sifa kugharimia masomo ya vyuo vya juu.

Na kimsingi walengwa wakiwa hasa wanafunzi wanaotoka katika familia maskini, ambazo hazina uwezo wa kulipia gharama za masomo yao.

Habari hizo zinatokana na malalamiko ya wanufaika ya namna deni linalotokana na mikopo waliyopewa, linavyozidi kuongezeka kila mwaka.

Linapaa kutokana na masharti ya vifungu vya mwongozo wa HESLB wa utoaji mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wanayoyaita ni ya ‘uonevu.’

Vifungu walivyovilalamikia ni pamoja na kile kinachowataka wanufaika kulipa tozo ya kulinda thamani ya fedha walizopewa, ambapo hukatwa asilimia sita kwa mwaka tangu tarehe mnufaika aliyoanza kupokea mkopo.

Vilevile kifungu kinachotaka bodi ikate asilimia moja ya ada ya uendeshaji kwa mnufaika.

Aidha, kifungu kinachoeleza kwamba iwapo mnufaika atashindwa kulipa mkopo baada ya kipindi cha neema cha miezi 24 akishahitimu masomo yake, ataongezwa makato ya adhabu ya asilimia 10.

Wanufaika wanabainisha kwamba vifungu hivyo vimekuwa shubiri kwao kiasi cha kuathiri ustawi wao kwa ujumla na kwamba kwa masharti hayo inaweza ikachukua hadi miaka 20 kwa wengine kumaliza madeni yao.

Muungwana ana imani kuwa maadamu serikali ya awamu ya tano ni sikivu, itakuwa imesikia kilio hiki.

Hata hivyo, Tulonge ambaye ni mmoja wa waumini wa usikivu wa serikali hii, anaishauri ichukue hatua moja mbele katika kushughulikia malalamiko ya wanufaika wa mikopo hii.

Kwamba kwa kuwa mikopo inatolewa hasa kwa watoto wanaotoka familia maskini ili kuwapa fursa ya kupata elimu ya juu, ni bora wanufaika wakalegezewa zaidi masharti ili lengo la kuwapa mikopo hiyo liwe na manufaa kwao.

Muungwana anashauri wanufaika watakiwe kurejesha kiasi cha fedha walizokopeshwa kugharimia masomo, bila ya tozo ama ada nyingine yoyote kama inavyofanyika sasa.

Msingi wa ushauri huu unajikita kwenye ukweli kwamba wengi wa wanufaika wanatoka familia maskini.

Hivyo kuwawezesha kupitia mikopo hii ni kama kuwanyanyua ili wapatapo ajira ama wanapojiajiri waweze kuziinua familia zao na hatimaye kuondokana na umaskini.

Sasa mnufaika anapotumia miaka zaidi ya 10 kurejesha mkopo aliopewa ukiambatana na makato ya ada na tozo, inakuwa ni kumpa mzigo wa kuufanyia kazi badala ya kuwa fursa ya kusaka maendeleo yake binafsi, familia, jamii na hatimaye taifa kwa ujumla.

Kwa maoni ya Muungwana, mantiki ya kumpa mkopo mnufaika inakuwa na nguvu zaidi pale anapowekewa mazingira mazuri baada ya masomo yake.

Mazingira hayo ni pamoja na kumtaka arudishe kiasi halisi cha mkopo aliopewa bila ya nyongeza.

Lakini msingi mwingine wa ushauri huu unatokana na ukweli kwamba elimu ni haki ya kila mtu kwa mujibu wa Katiba, na serikali ina wajibu wa kuhakikisha watu wote wanapata fursa sawa na za kutosha kuwawezesha kupata elimu.

 Na ndiyo maana inatoa elimu bure kuanzia shule za awali hadi kidato cha nne ili kutimiza moja ya majukumu yake ya kikatiba kwa wananchi wake.

Hivyo kuwapa fursa wanufaika ya kurejesha kiasi halisi cha fedha walizokopeshwa bila ya ada na tozo zingine, ni suala la kikatiba vilevile.

Aidha, ni ukweli vilevile kwamba, serikali haifanyi biashara katika elimu na ndiyo maana imeondoa ada na tozo zilizokuwa zikitozwa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Sasa kuweka ada na tozo kwa wanufaika wa mikopo elimu ya juu ni sawa na serikali kufanya biashara katika elimu kwa maoni ya Muungwana.

Habari Kubwa