Jamii ichukue hatua kulinda maadili ya wanafunzi shuleni

28Aug 2019
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
Jamii ichukue hatua kulinda maadili ya wanafunzi shuleni

KATIKA mfumo wa maisha huwa ni jambo la kawaida mtoto kutunzwa au kulelewa na wazazi hata na ndugu akielekezwa kuzingatia maadili mema, ambayo yanalenga kumfanya awe mtu mwema katika jamii.

Hivyo iwapo watoto watazingatia mfumo huo wa malezi, mwisho wa siku wanaweza kuwa raia wema na wenye manufaa kwa familia zao, jamii na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, mfumo unazidi kubadilika kutokana na migongano ya maisha, uchumi duni, umaskini, ufukara na utandawazi katika zama hizi, hatua inayosababisha madhara makubwa kwa watoto.

Miongoni mwa madhara hayo ni mmomonyoko wa maadili, unaosababisha watoto wakiwamo wanafunzi kujiingiza katika vitendo vibaya vinavyoweza kuwaharibia ndoto zao za baadaye.

Wiki iliyopita, wadau mbalimbali wa maendeleo ya mtoto walikutana katika warsha iliyolenga kuwa na mkakati wa kutambua mbinu za kuwasiliana kwa ajili ya kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto.

Warsha hiyo ilioandaliwa na taasisi ya Ekama Development Foundation Tanzania, ilishirikisha wadau 120 ambao ni wanafunzi, walimu, wazazi, viongozi wa serikali za mitaa kutoka wilaya za Temeke na Kigamboni.

Ilidaiwa na baadhi ya wanafunzi na walimu kwamba wapo baadhi ya wanafunzi ambao hufanyiana vitendo vya ukatili (kulawitiana) wenyewe kwa wenyewe.

Kutokana na madai hayo, viongozi wa dini waliombwa kusaidia kukemea mmomonyoko wa maadili ili jamii ilirudi kwenye mstari unaozingatia malezi mema badala ya kukaa kimya huku watoto wakiendelea kuharibika.

Ofisa Elimu ya Msingi wa Wilaya ya Temeke, Mectilda Rukoijo, anasema mmomonyoko wa maadili kwa vijana, hasa wanafunzi wa shule za msingi usipodhibitiwa kikamilifu utasababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kuwa na taifa lisilo na maadili.

Muungwana anawaasa wazazi kutafakari mienendo yao ili kumaliza tatizo hili ambalo linakwenda kinyume na maadili.

Kuwapo kwa vitendo hivyo vya mmomonyoko maadili shuleni maana yake ni kwamba chanzo kipo, hivyo ni wajibu kwa wazazi kutafakari mienendo yao au malezi yao kwa watoto.

Pamoja na kwamba juhudi mbalimbali za kulinda maadili zimekuwa zikichukuliwa na wadau mbalimbali wa haki za watoto, bado wazazi wana sehemu kubwa ya malezi bora kwa watoto wao.

Wazazi wasipochukua hatua kwenye suala hili wanaweza kusababisha vijana wao kujikuta wakiwa na maambukizi ya virusi ya Ukimwi, kwani tatizo hilo ni kubwa haliwezi kufumbiwa macho.

Kila mzazi anatakiwa kufuatilia na kujua mwenendo wa mtoto wake na kuurekebisha pale anapoona unakwenda kinyume kwani shule ni sehemu ya kupata elimu, si kufanyia mambo ya mmomonyoko wa maadili.

Sidhani kwamba wazazi na walezi wanaweza kukwepa lawama au kujitetea katika hili kwani ni muhimu ijulikane wanakojifunzia vitendo hivi watoto wao.

Kama watoto wanaachwa huru kupita kiasi, basi wazazi wajue kuwa mtindo huo unachangia kuwapo kwa vitendo hivyo, ambavyo kama nilivyosema, madhara yake ni makubwa kwa maisha yao ya baadaye.

Kwa mazingira ya aina hiyo, ipo haja sasa wazazi kuwakagua watoto wao mara kwa mara kwani wanaweza kufanyiwa ukatili na mtu wa karibu au wenzao shuleni na kujikuta wakiharibika.

Wazazi ni nguzo muhimu ya malezi kwa watoto wao, lakini yanapolega, maana yake ni kuharibika kwa mtoto.

Muungwana anatafakarisha kwa mfano suala la baadhi ya wazazi kulala chumba kimoja na watoto wao wakubwa, nini hatma yake?

Wengine wanaacha watoto wakiangalia hata picha za ovyo kwenye vibanda vya kuonyeshea video mitaani na kwa mazingira kama hayo ni lazima vitendo vya mmomonyoko wa maadili vitatokea.

Viongozi wa dini wana umuhimu wao katika suala zima la kukemea tabia hiyo ili kulinda watoto dhidi ya mmomonyoko, ambao unaweza kusababisha kukawa na taifa bovu la baadaye.

Habari Kubwa