Kila raia kuwa na bima kuanze sasa

30Aug 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kila raia kuwa na bima kuanze sasa

KATIKA siku za hivi karibuni kumekuwapo na mijadala mbalimbali inayohusisha umuhimu wa kuwapo kwa utaratibu wa kutumika kwa bima ya afya kwenye matibabu ya Watanzania wote.

Hoja hizo zinakuzwa na taarifa za kuwapo kwa kilio cha wagonjwa wanaoshindwa kumudu gharama za matibabu kutokana na uwezo mdogo na kutokuwapo kwa mfumo wa bima ya afya unaowanufaisha wengi.

Tukisema walio wengi tunamaanisha mifumo ya sasa inawalenga na kuwahudumia zaidi walio kwenye ajira rasmi ama ndani ya sekta ya umma au binafsi.

Taarifa za kutoka vyanzo mbalimbali zikiwamo za Wizara ya Afya, zinaonyesha kuwa ni wastani wa asilimia saba pekee ya Watanzania walio katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Aidha, zinasema ni wastani wa asilimia 13 hadi 15 pekee ya Watanzania ndiyo waliopo kwenye mfumo wa bima ya afya, hii ikihusisha mifumo mingine kama ile inayohudumia wateja kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF.

Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi hugharamia matibabu kwa kulipa fedha za tiba kila wanapougua.

Ukubwa wa tatizo hili huonekana kuwa kubwa zaidi pale panapotokea magonjwa yanayohitaji vipimo na uchunguzi wa gharama zaidi, wengi hushindwa kugharamia tiba kwa kukosa fedha mifukoni.

Changamoto za kukosekana utaratibu wa bima ya afya unaowahudumia Watanzania wengi umeonekana mara nyingi wagonjwa wanapoomba msaada wa kuchangiwa malipo au fedha kwa ajili ya matibabu iwe ndani au nje ya nchi.

Tatizo hilo linatokana na ukweli kwamba hakuna mifumo imara ya ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya kuchangia matibabu ambazo kila mmoja anawekeza kwenye mifuko rasmi ya tiba kupitia bima.

Wakati watumishi wa umma na wachache kutoka sekta binafsi ndiyo waliojiunga kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wakulima, wamachinga na wanaoishi vijijini baadhi yao wanatibiwa kupitia Mifuko ya Bima ya Jamii (CHF) ambayo sasa huitwa CHF iliyoboreshwa.

Hata hivyo, kiwango cha wanufaika wa huduma za bima nchini ni kidogo na serikali mara kwa mara inasema inaandaa utaratibu wa kuanzisha kwa bima ya afya ya wote.

Kufanikiwa kutekelezwa kwa mpango huo kutapunguza changamoto za matibabu kwa wananchi wengi na kutokana na kuongezeka kwa magonjwa mengi hasa yaliyosugu na yasiyoambukiza ambayo humwandama mgonjwa katika kipindi chote cha uhai wake.

Tunaamini hili ni suala la msingi na la muhimu kutokana na ukweli kwamba sekta ya tiba imeboreshwa kwa kiwango kikubwa na kuongeza huduma nyingi za kibingwa zenye kuhitaji vipimo vikubwa ambavyo miaka ya nyuma hazikuwa zikipatikana hapa nchini.

Huduma hizo zimesababisha gharama za vipimo kuwa kubwa zaidi zikilinganishwa na kipato cha Mtanzania.

Huduma hizo kama kuchunguzwa moyo, kupandikiza figo, kufanyiwa vipimo na tiba za mifupa, mishipa ya fahamu na ubongo zinapatikana Muhimbili, lakini malipo yake ni makubwa.

Tunaona kuwa bila bima ya afya ni wachache wanaoweza kujigharamia.

Ndiyo maana wakati serikali ikijipanga kuhakikisha wananchi wanajiunga kwenye mifumo rasmi ya bima za matibabu inapaswa kuongeza na kuimarisha elimu ya bima ya afya kwa wananchi ili kuwahamasisha umuhimu wa kujiunga.

Ndiyo maana tunaona kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, anapozungumzia kwa msisitizo kuwa ni vyema kila Mtanzania kuwa na bima ya afya ni suala linalopokelewa na mikono yote.

Tunaungana naye tukisema hatua hizo zitanusuru taifa kutokana na mzigo mzito wa kugharamia tiba unaoiathiri jamii yetu.

Habari Kubwa