Yanga, Zahera ushirikiano unahitajika kuitoa Zesco

31Aug 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga, Zahera ushirikiano unahitajika kuitoa Zesco

HATIMAYE Tanzania Bara imebakiwa na timu mbili tu kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya wawakilishi wawili, Simba na KMC FC kutolewa kwenye raundi ya awali.

Kwa sasa macho na masikio yote kwa Watanzania yameelekezwa kwa Yanga inayoiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa na Azam FC inayopeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba ambayo msimu uliopita ilifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwenye michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf), imeyaaga mashindano hayo baada ya kutolewa kwa faida ya bao la ugenini na UD Songo ya Msumbiji kufuatia sare ya bao 1-1 ikiwa ni baada ya awali kutoka suluhu.

Kwa upande wa KMC FC ambayo hii ilikuwa ni mara ya kwanza kupanda Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kufanikiwa kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, yenyewe imetolewa na AS Kigali ya Rwanda kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya mechi ya awali ugenini kutoka suluhu.

Aidha, Yanga ambayo imeitoa Township Rollers ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1 kufuatia sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda kushinda kwa bao 1-0 ugenini, sasa itakabiliana na Zesco ya Zambia katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo.

Hivyo, Yanga inahitaji maandalizi makubwa ili kuweza kuitoa Zesco ambayo iliitoa Green Mamba FC ya Eswatini kwa jumla ya mabao 3-0, wakati pia Azam FC iliyoitoa Fasil Kenema ya Ethiopia kwa mabao 3-2, inapaswa kufanya kazi ya ziada kuitupa nje Triangle FC ya Zimbabwe iliyoiondosha Rukinzo FC ya Burundi kwa jumla ya mabao 5-0.

Hakika haitakuwa kazi rahisi kwa wawakilishi wetu hao waliosalia kwenye michuano hiyo, ambayo tunatamani kuwaona wakisonga mbele ili kuweza kuiongezea pointi Tanzania na kufanikiwa kuingiza tena timu nne kwenye michuano hiyo ya Caf msimu ujao.

Na wakati huu timu hizo zikijiandaa kuelekea mechi hizo, tungependa kuona viongozi wa klabu hizo wakizingatia zaidi progamu ya mazoezi ya makocha ili kuondoa lawama pindi timu zinapofanya vibaya.

Tumelazimika kukumbusha suala hilo, kutokana na ukweli kwamba, kabla ya Yanga kuelekea Botswana kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Township Rollers, iliweka kambi mikoa ya Kaskazini, Kilimanjaro na baadaye Arusha na kisha kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania na AFC Leopards ya Kenya.

Hata hivyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera alilalamikia kambi hiyo akidai kwamba haikuwa na maslahi ya kuwasaidia wachezaji na badala yake uongozi ulilenga kujiingizia kipato zaidi badala ya kumulika kuiandaa timu kutokana na mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Township Rollers iliyokuwa ikiwakabili.

Zahera alienda mbali zaidi kwa kueleza kuwa alishindwa kuwachezesha wachezaji wake muhimu katika mechi hizo za kirafiki kutokana na viwanja vibovu jambo ambalo alihofia wanaweza kuumia na kumgharimu kuelekea mechi hiyo ya marudiano.

Ni wazi kabisa, kama Yanga ingepoteza mchezo huo Zahera tayari alishapata sababu ya kujitetea, jambo ambalo hata hivyo liliepukika kutokana na timu hiyo kushinda na kufanikiwa kusonga mbele.

Septemba 13, mwaka huu siku ambayo mechi ya kwanza kati ya Yanga na Zesco itapigwa Uwanja wa Taifa, si mbali, hivyo maandalizi ya kina yanahitajika na umoja kati ya uongozi wa klabu hiyo na benchi la ufundi.

Hatutarajii tena kusikia kukiwapo na kutupiana lawama kati ya benchi la ufundi na uongozi wa Yanga, kwani lengo letu ni kuona Yanga na Azam zikifika mbali katika michuano hiyo ili Tanzania iweze kuingiza tena timu nne kwenye michuano hiyo msimu ujao.

Na hilo litawezekana tu kama kwa wiki hizi mbili maandalizi ya kina kwa kila timu yatafanyika na kwa upande wa Yanga ikimulika zaidi safu yake ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikikosa mabao mengi katika mechi za kimashindano na za kirafiki ilizocheza hadi sasa.

Habari Kubwa