Yanga: Hakuna kapa isiyokuwa na usubi

31Aug 2019
Barnabas Maro
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga: Hakuna kapa isiyokuwa na usubi

‘USUBI’ ni wadudu wadogo wanaofanana na mbu. ‘Kapa’ ni sehemu ya pwani inayoota mikoko na ambayo huwa na tope na haikosi usubi. Maana yake hakuna msitu wa mikoko usiokuwa na usubi.

Methali hii yatufunza kuwa hakuna kitu kisichokuwa na kasoro au hitilafu zake. Kila kitu kina faida na hasara zake.

Tangu Yusuf Manji alipojiuzulu Uenyekiti wa Yanga, klabu hiyo kongwe ni kama ilifiwa na mlezi wake kwani aliiacha katika ufukara mkubwa. Hali hiyo iliiweka Yanga kwenye matatizo makubwa ya fedha hata kushindwa kulipa mishahara ya wachezaji na stahiki zao, kadhalika watumishi wengine wa klabu.

Wanachama na mashabiki wa Yanga hawakukubaliana na Manji kujitoa kwenye uongozi lakini yeye alisimama kidete kutetea msimamo wake. Jambo hilo lilisababisha klabu ya Yanga ishindwe kujiendesha yenyewe hata kuitwa ‘ombaomba’ (hali duni inayohitaji msaada kutoka kwa wengine).

Watani zetu (Simba) wakawa wanawatania kwa kuwaita ‘Yanga bakuli’ yaani wanaopita na bakuli mitaani na viwanjani kuomba msaada. Hata Yanga ilipokuwa inapambana na timu zingine, wapiga picha za runinga hawakukosa kuonesha picha za watu waliokuwa wakichangisha fedha kwa ajili ya Yanga.

Ilikuwa fedheha ya aina yake kwa klabu kongwe kuomba msaada viwanjani. Ni jambo lililokera wengi, lakini hakukuwa na jinsi ila kukubaliana na hali halisi.

Hata hivyo, wahenga walisema: “Hakuna kubwa lisilo ukomo.” Maana yake kila jambo lina mwisho wake kwani hata maisha ya binadamu hufikia kikomo chake. Methali hii hutumiwa kumliwaza mtu anayepambana na hali ngumu au matatizo kuwa ajitahidi kuvumilia hatimaye yatafikia mwisho wake.

Hivi karibu, wanachama wa Yanga walifanya uchaguzi na kumchagua Dk. Mshindo Msolla kuwa Mwenyekiti wao kwa kumpa kura 1,276 huku mgombea mwenzake wa nafasi hiyo, Dk. Jonas Tiboroha aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa Yanga enzi za Mwenyekiti Yusuf Manji, akipata kura 60 tu.

Hata hivyo, ingawa Dk. Jonas Tiboroha alishindwa, alikubali matokeo ya uchaguzi huo na kumtaka Mwenyekiti mpya (Dk. Msolla) avunje makundi kama alivyoahidi wakati akijinadi. Akasema kwa roho nyeupe amekubaliana na matokeo na kutoa rai kuwa kambi zote zivunjwe ili Yanga iwe moja chini ya Mwenyekiti Dk. Mshindo Msolla.

 Aliyeshinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Fredrick Mwakalebela aliyewashinda wagombea wengine watano kwa kupata kura 1,206. Mwakalebela alipata kuwa Katibu Mkuu wa TFF zamani. Walioshinda nafasi za ujumbe ni: Frank Kamugisha, Arafat Haji, Salum Rupia, Bahati Mwaseba, Saad Kimji, Rodgers Gumbo, Ahmad Islam na Dominic Kata.

Viongozi hawa wameitwaa Yanga ikiwa na matatizo mengi yanayohitaji hekima, maarifa na juhudi kubwa kuirejesha pale ilipokuwa zamani. Kama kuna kiongozi aliyechaguliwa kwa lengo la kujinufaisha badala ya kuinufaisha Yanga, ni vema ajiondoe mapema na kuwaachia wenye uchungu na Yanga, wenye lengo la kuitoa kwenye umasikini uliokithiri.

Viongozi wapya wanapaswa kuzingatia mambo makubwa manne.  Wahakikishe wanapata hatimiliki (waraka wa kisheria unaompa mhusika haki ya kumiliki ardhi au mali nyingine) iliyo mikononi mwa mtu asiyetaka kuipa klabu. Kama atakataa kuitoa kwa viongozi, ashitakiwe mahakamani ili haki itendeke ili hatimiliki irejeshwe klabuni.

Hatimiliki hiyo itumiwe na viongozi kama dhamana ya kupata mkopo wa Benki itakayokubali kujenga ile nyumba iliyokuwa makao makuu ya Yanga zamani kwenye makutano ya mitaa ya Mafia/Nyamwezi jijini Dar es Salaam. Jengo hilo laweza kuwa la ghorofa 10 au zaidi, maalum kwa biashara kama hoteli na maduka, likiwamo duka la klabu litakalouza jezi, skafu, vikombe vya chai, glasi na vifaa mbalimbali vya michezo vyenye nembo ya Yanga.

Pili lile ghorofa linalotumika sasa kule Jangwani, lifanyiwe ukarabati mkubwa ili liwe maalum kwa ofisi za viongozi wa klabu na pia malazi ya wachezaji wanapokuwa kambini badala ya kukodi hoteli za watu binafsi kama ilivyozoeleka.

Ghorofa ya chini iwe mahsusi kwa wachezaji kupata chakula, vinywaji baridi na eneo maalum la kuwapa wachezaji mafunzo ya nadharia (maelezo ya kanuni na namna ya kufanya jambo fulani) kwa muktadha huu, kandanda. 

Tatu, viongozi wapya wafute kabisa mpango wa ujenzi wa uwanja wa mpira pale Jangwani kwani ni eneo linalofurika maji wakati wa mvua za masika na vuli. Ni eneo ambalo chini yake kuna bomba kubwa la maji yanayokwenda kwenye Hospitali Kuu ya Rufani Muhimbili. Kwa ufupi wakubaliane na maelezo ya serikali kuwa eneo lile halifai kujengwa uwanja wa mpira.   

Kwa kuwa wakati wa mvua ndio mujarabu kujua eneo zuri la kujenga viwanja vya mpira, viongozi watembelee maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na viunga vyake ili kujua maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa viwanja vya michezo kwani hayatakuwa yamejaa au kuzungukwa na maji ya mvua.

Jambo la nne: Viongozi wapya wawaondoe ‘makomandoo’ kwani ndio wanaotumiwa na viongozi ‘wachumia tumbo’ wanaojitafutia shibe kwa kuinyonya Yanga. ‘Makomandoo’ hujifanya ndio wanaoijua Yanga na kuipenda sana kumbe ndiko wanakoshibia!

Viongozi wapya wasikubali kupokea taarifa za maneno kutoka kwa watangulizi wao bali kila kitu kifanyike kwa maandishi. Ikiwezekana, vitabu vya hesabu vipelekwe kwa wakaguzi ili vikaguliwe kujua fedha zilizoingia, na kazi zilizofanyia. Endapo kutakuwa na shaka, wahusika washitakiwe ili sheria ifuate mkondo wake.

Dk. Msolla na wenzake wafanye juhudi kuifanya Yanga iwe kampuni na kuwa klabu yenye hisa kwani “Hakuna kubwa lisiloshindwa.” Maana yake hakuna jambo lisilowezekana. Hutumiwa kumhimiza mtu anayekabiliana na hali ngumu kuwa lazima atafanikiwa hatimaye.

Habari Kubwa