Stars malizieni kazi Burundi

02Sep 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Stars malizieni kazi Burundi

TIMU ya Tanzania, 'Taifa Stars' keshokutwa itashuka dimbani nchini Burundi kumenyana na wenyeji wao hao kwenye mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.

Taifa Stars itashuka dimbani ikiwa na morali wa kuendelea kufanya vizuri kutokana na mwezi uliopita kuitoa timu ya Taifa ya Kenya, 'Harambee Stars' kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kufuzu fainali za Wachezaji wa Ndani, CHAN.

Sasa Stars inasubiri kuvaana na Sudan na kama itaitoa itafuzu moja kwa moja kushiriki fainali hizo za CHAN zitakazofanyika mapema mwakani nchini Sudan. Na kama Stars itafuzu huu utakuwa mwaka wa mafanikio kwa Tanzania baada ya Juni mwaka huu kushiriki kwa mara ya kwanza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) nchini Misri tangu 1980.

Hata hivyo, kwa michuano ya CHAN kama Stars itafuzu hii itakuwa mara ya pili kushiriki fainali hizo kwani ilishiriki kinyang'anyiro hicho mara ya kwanza ilipoanzishwa mwaka 2009.

Hivyo, wakati huu Stars ikielekea kuivaa Burundi, inapaswa kupigana kufa au kupona ili kumaliza kazi kwenye mechi hiyo ya kwanza ugenini na isisubiri kukutana na presha ya mchezo wa marudiano kama ilivyokuwa dhidi ya Harambee Stars kuwania kufuzu CHAN.

Tunasema hivyo kutokana na mechi ya kwanza Uwanja wa Taifa dhidi ya Harambee Stars, Taifa Stars ililazimishwa sare kabla na yenyewe kwenda kulazimisha sare ugenini nchini kwao na kuwatoa Wakenya hao kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

Hivyo, Taifa Stars haina budi kutambua biashara ni asubuhi na inapaswa kumaliza kazi mapema na kutosubiri kutegemea kushinda nyumbani wakati wa mechi ya marudiano Septemba 8, mwaka huu Uwanja wa Taifa.

Ushindi katika mechi hiyo ya ugenini itaifanya Stars kucheza kwa kujiamini zaidi katika mechi ya marudiano nyumbani huku presha ikiwa kwa Burundi ambayo itakuwa ikihitaji kupindua matokeo.

Tunatambua kikosi kilichoitoa Harambee Stars CHAN kitakuwa kimeongezewa nguvu kubwa kutoka kwa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi akiwamo nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta, anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji.

Kwa mantiki hiyo Kaimu Kocha Mkuu, Mrundi Etienne Ndayiragije keshokutwa, Jumatano atakuwa na uwanja mpana zaidi wa kupanga kikosi kitakachompa matokeo chanya kwa kuwa silaha zake zimeongezeka.

Aidha, uwapo wa Ndayiragije unatupa matumaini zaidi ya kufanya vizuri katika mechi hiyo kwani atakuwa anayaelewa vema mazingira na falsafa za soka la kwao Burundi.

Lakini pia Ndayiragije atataka kushinda mchezo huo ili kulionyesha Shirikisho la Soka la Burundi, kuwa limefanya makosa kwa kutompa nafasi ya kukinoa kikosi hicho cha timu yao ya Taifa, hivyo ushindi si faida tu kwa Stars bali pia kwa kuongeza wasifu wa kocha huyo.

Kwetu sisi Nipashe tunaungana na Watanzania wengine kuiombea Stars ipate matokeo chanya ugenini kabla ya kurejea nyumbani kukamilisha tu ratiba katika mechi ya marudiano Jumapili ijayo.

Tunaitakia kila la heri katika mechi hiyo, lakini pia tukiwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kusafiri kuelekea Burundi kuishangilia Taifa Stars katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali kwa pande zote.

Habari Kubwa