Kocha wa makipa Simba ajitazame kwenye kioo

02Sep 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kocha wa makipa Simba ajitazame kwenye kioo

NAKUMBUKA baada ya Ligi Kuu kumalizika nilisoma mahali jinsi Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems alivyokuwa akitoa tathmini yake kwenye kikosi chake, benchi la ufundi, pamoja na ushauri jinsi gani ya kuboresha kwa ajili ya msimu huu.

Moja ya yale aliyosema ni kwamba alikuwa akichukizwa na makipa wake Aishi Manula na Deogratius Munishi 'Dida' kufungwa mabao ya aina moja.

Akiwa na maana kuwa makipa wake wanafungwa mabao yanayofanana. Aliyokuwa akifungwa Manula, siku akiwekwa Dida naye anafungwa kwa staili ile ile kama ya mwenzake.

Hilo lilionekana kumkera na kuahidi kulitafutia dawa ya kutafuta kocha wa makipa na aliyekuwapo aende kuongeza ujuzi.

Hata hivyo, msimu umeanza kocha wa makipa ni yule yule Muharami Mohamed, kipa mahiri wa zamani wa Simba, Pan Africa, Taifa Stars na pia amecheza soka la kulipwa nchini Msumbiji.

Ukiangalia mechi nyingi za msimu uliopita za Ligi Kuu, makipa wa Simba walikuwa wakifungwa mabao ya mbali na krosi.

Mastraika wanaopiga mipira kuanzia mita 20 kurudi nyuma wakiwa na asilimia kubwa ya kuwafunga kama mpira hiyo italenga goli. Hii iliwaweka roho juu wanachama na mashabiki wa Simba wanapoangalia mechi zao.

Lakini hata wachezaji waliokuwa wakicheza na Simba walionekana mkazo wao zaidi ni kupiga mashuti ya mbali. Na kuna wakati walifanikiwa.

Wanachama na mashabiki walipiga kelele sana juu ya makipa wa Simba kufungwa mabao ya aina hiyo. Msimu huu Simba imemsajili mmoja wa makipa wazuri kabisa nchini, Beno Kakolanya.

Hakuna shabiki yeyote yule nchini ambaye hajui umahiri wa Kakolanya. Kwenye mechi dhidi ya Azam katika namna ya kushangaza, naye alifungwa mabao mawili ya mbali kama yale yale ambayo Manula amekuwa akifungwa.

Alhamisi iliyopita, Manula alifungwa bao la takriban mita 24 kwenye mechi dhidi ya JKT Tanzania. Licha ya kushinda mabao 3-1, lakini bao hilo lilizua mjadala mkubwa mitaani na kwenye mitandao ya kijamii.

Sidhani kama inahitaji mjadala, badala yake imeshazoeleka kuwa makipa wa Simba wamekuwa na tatizo hilo.

Hata kama akitoka kwenye timu nyingine akiwa hafungwi mabao ya mbali, lakini anapoingia kwenye klabu hiyo naye anakuwa kama ameambukizwa tatizo hilo hilo.

Klabu ya Simba inaonekana kusajili makipa ikitegemea kutibu baadhi ya mapungufu walionayo makipa wao, lakini kipa anayesajiliwa naye anakuja kuwa na mapungufu yale yale ya wenzake.

Kwa maana hiyo tatizo halitokuwa la makipa hao. Lipo kwenye benchi la ufundi na hasa kocha wa makipa. Ilitegemewa baada ya ligi kumalizika, msimu huu kocha wa makipa angekuwa na mbinu mbadala, au kuwa ameshapata mwarobaini wa hilo, lakini kwenye mechi za awali tu imeonekana kuwa tatizo hilo bado liko pale pale.

Manula na Kakolanya ni makipa wakubwa na tegemeo kwa nchi yetu kwa sasa. Kufungwa mabao ya mashuti ya mbali si aibu kwao tu, bali pia hata kwa kocha wao anayewafundisha.

Ni kwa sababu makipa hawa wote huko walikotoka, Yanga na Azam hawakuwa na matatizo hayo. Muharami anatakiwa aliangalie hili kwa sasa kwani bado wanachama na mashabiki wengi wanaona safu yao ya ulinzi ni tatizo. Lakini likishaonekana kuwa limetibika na makipa wake wakaendelea kutunguliwa na mashuti ya mbali, mjadala utahamia kwake.

Habari Kubwa