Bugando mbioni kuanzisha matibabu magonjwa ya moyo

02Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
MWANZA
Nipashe
Bugando mbioni kuanzisha matibabu magonjwa ya moyo

HOSPITALI ya Rufani ya Kanda Bugando mkoani Mwanza, inatarajia kuanzisha kituo cha taasisi ya kutoa huduma za magonjwa ya moyo, kitachogharimu kiasi cha Sh. bilioni 59.

kurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Prof. Abely Makubi.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Prof. Abely Makubi, katika hafla fupi ya uzinduzi wa wodi vyumba 18 vya watu mashuhuri (VIP) na wodi vyumba vinane vya binafsi  pamoja na vitanda 38.

“Bugando tunatarajia kuanzisha kituo cha taasisi ya Moyo kwa ajili ya kutoa huduma za upasuaji magonjwa ya moyo na mafunzo, ambacho kitajengwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya, wadau wa Mwanza, wafadhili wa nje na Kanisa Katoliki, alisema Prof. Makubi.Katika uzinduzi huo Prof. Makubi alisema Sh. milioni 230 zimetumika kujenga vyumba hivyo 18 vya wodi za VIP na Sh. milioni 132 zimetumika kujenga vyumba vya wodi binafsi vinane na huduma ya vitanda 38.

Hospitali hiyo imekuwa mtoaji mkubwa wa misaada kwa wagonjwa wasiojiweza, ambayo kila baada ya miezi mitatu hutumia Sh. milioni 420 sawa na Sh. milioni 140 kila mwezi kuhudumia bure wagonjwa wasiojiweza.“Kila baada ya miezi mitatu tunatumia fedha nyingi kuhudumia wagonjwa maskini wasiojiweza ambao ni wajawazito, watoto chini ya umri wa miaka mitano na wazee kuanzia miaka 60 na kuendelea,” alisema Prof. Makubi.

Alisema kuwa sambamba na kuboreshwa kwa mazingira ya hospitali hiyo na vifaa tiba, pia imeongeza madaktari bingwa na waliobobea katika magonjwa mbalimbali wakiwamo wazalendo na madaktari bingwa kutoka Nepali na Cuba.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliwataka wananchi wa mkoa huo kujiandikisha katika huduma ya bima ya afya.

Habari Kubwa