Dulla Mbabe kutua leo na ubingwa wa WBO

02Sep 2019
Shufaa Lyimo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Dulla Mbabe kutua leo na ubingwa wa WBO

BAADA ya kufanya kweli kwa kuipeperusha vema bendera ya Tanzania nchini China kwa kumtwanga kwa Knockout (KO) raundi ya tatu mwenyeji, Zulipikaer Maimaitiali, bondia Mtanzania, Abdallah Shaaban Pazi-

bondia Mtanzania, Abdallah Shaaban Pazi ‘Dulla Mbabe’.

-‘Dulla Mbabe’ anatarajiwa kuwasili nchini leo asubuhi akiwa na taji lake la ubingwa wa WBO Asia Pacific uzito wa Middle.

Katika pambano hilo lililopigwa juzi kwenye Ukumbi wa TSSG Center mjini Qingdao, China, Dulla Mbabe alilianza kwa kasi na kumpelekea makonde mfululizo Zulipikaer, ambaye ni bondia namba moja China na aliyekuwa akishikilia mkanda huo, kabla ya kumkalisha chini raundi ya tatu.

Akizungumza na Nipashe juzi akiwa nchini humo Dula Mbabe alisema ameshukuru kupata ubingwa huo aliokuwa anautamani kwa muda mrefu, alisema licha ya pambano hilo kuwa gumu na lenye ushindani mkubwa alijituma mpaka kuhakikisha anapata ushindi huo ugenini.

"Mpambano ulikuwa mgumu, lakini nashukuru nimejitahidi nimepata ubingwa ambao umetokana na dua za Watanzania," alisema Dulla.

Aliwataka Watanzania pamoja na mashabiki wa mchezo huo kujitokeza kwa wingi leo asubuhi katika Uwanja wa Ndege Julius Nyerere sasa tatu asubuhi kumpokea kufuatia kuipeperusha vema bendera ya nchi kwenye medali ya masumbwi.

Kwa upande wake promota wa Dulla Mbabe, Jay Msangi, alisema kijana wake ameliletea sifa taifa lake, Tanzania kwa ushindi huo.

“Ni heshima kubwa, wadau tujitokeze kwa wingi kwenye hafla ya kumpokea bingwa huyu siku ya Jumatatu saa tatu na nusu asubuhi pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,” alisema Jay Msangi.

Kwa ushindi huo, sasa Dulla Mbabe anashikilia mataji mawili makubwa, lingine ni la WBF Intercontinental uzito wa Super Middle baada ya kumpiga Mtanzania mwenzake, Francis Cheka kwa KO pia raundi ya sita Desemba 26, mwaka jana katika Ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa