Simba yaja na mkakati mpya

02Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba yaja na mkakati mpya
  • ***Mo amwaga sera, Kagere kuletewa wembe mpya unaomzidi kucheka na nyavu huku ikielezwa...

WAKATI Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba Mohammed ‘Mo’ Dewji amewataka wapenzi na wanachama wa klabu hiyo kuwa wavumilivu baada ya timu yao kutolewa mapema katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika imefahamika miamba hiyo imeelekeza nguvu zake kusaka straika zaidi ya Meddie Kagere

Mabingwa hao wa Tanzania, Simba wametupwa nje mapema kwenye raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kulazimishwa sare ya bao 1-1 na UD Songo ya Msumbiji katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni baada ya mechi ya awali ugenini kulazimisha suluhu, hivyo kutolewa kwa faida ya bao la ugenini.

Kwa kipindi chote tangu Simba kutolewa Jumapili ya Agosti 25, mwaka huu, uongozi wa klabu hiyo ulikuwa kimya huku mashabiki wa timu hiyo wakishindwa kuelewa kinachoendelea.

Lakini Jumamosi Mo, aliibuka na kuwataka Wanasimba kuwa wavumilivu baada ya timu yao kutolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa, huku taarifa zaidi kutoka chanzo chetu ndani ya klabu hiyo zikieleza hasira yao sasa ni kutafuta straika zaidi ya Kagere.  

“Wanasimba, mnisamehe kwa ukimya. Maumivu ya matokeo yametupata sote. Naomba tukumbushane, sisi ni Simba! Simba lazima anyanyuke! Hawezi kukata tamaa. Niwaombe tusivunjike moyo wala kukata tamaa. Hatutaogopa maneno ya watu na hatutaacha kupambana na kujipanga kwa ajili ya malengo yetu,” alisema Mo kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Alisema msimu huu watautumia kikamilifu kuhakikisha wanaboresha mipango yao ili msimu ujao warudishe furaha ya wapenzi wa klabu hiyo.

“Tumwombe Mwenyezi Mungu atutangulie katika safari yetu endelevu. Tukumbushane tena: Roma haikujengwa kwa siku moja. Tuwe wavumilivu, tutafika tu Insha’Allah,” alisema.

Hata hivyo, chanzo chetu kilieleza: "Unajua kwa ujumla uongozi umeumia sana kutokana na matokeo hayo, na umeona kuna haja ya kutafuta straika mwenye uwezo kama ama zaidi ya Kagere kwa kuwa tatizo lilionekana katika safu ya ushambuliaji.

"Hata kocha Aussems [Patrick], alisema mara tu baada ya ligi ya msimu uliomalizika kuwa anahitaji straika zaidi ya Kagere, lakini uongozi haukulifanyika kazi ipasavyo, jambo ambalo limeonekana wazi kwenye mechi dhidi ya UD Songo.

"Shida ni pale mabeki wa upinzani wanapobaini straika pekee na wembe ni Kagere, ndiye anayepelekewa mipira, hivyo anapobanwa biashara inakuwa imekwisha, na ukitazama mechi iliyopita Bocco [John] alikuwa majeruhi," kilisema chanzo chetu.

Aidha, kilifafanua kuwa mchakato huo utafanywa kipindi cha dirisha dogo ili kutoa nafasi kwa straika huyo kuanza kuzoeana na wachezaji wenzake kabla ya msimu ujao kuanza.

"Lengo kwa sasa Simba inataka kujenga timu itakayokaa na wachezaji wake kwa muda mrefu, waweze kuzoeana tayari kwa msimu ujao, hilo ndilo unaolitaka uongozi kwa sasa," kilisema chanzo hicho.

Msimu uliopita Simba ilitinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa lakini moja ya makosa yanayoelezwa kufanya ni kuacha baadhi ya wachezaji wake nyota, kama kiungo James Kotei na beki Juuko Murshid kuondoka huku wachezaji wapya waliosajiliwa wakichelewa kuzoeana na wenzao.

Habari Kubwa