Rasilimali madini yaibua maswali Same

03Sep 2019
Godfrey Mushi
SAME
Nipashe
Rasilimali madini yaibua maswali Same

UTAJIRI wa madini ya vito ya green na red tormeline, rubi na dhahabu katika Wilaya ya Same, unaacha maswali lukuki ya kwa nini bado wananchi wake wanaishi katika lindi la umaskini, licha ya kugunduliwa idadi kubwa ya madini ya aina mbalimbali.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, Rosemary Senyamule.

Juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, Rosemary Senyamule, alithibitisha kugunduliwa kwa aina mpya ya madini ya green na red tormeline.

“Ni kweli mimi na kamati yangu, tumekwenda kujiridhisha kwa kutembelea maeneo mbalimbali yanayopatikana madini kama green na red tormeline, bauxite, almandite, blue sapphire na zilicon,” alisema.

Maeneo yaliyogunduliwa kuwa na utajiri wa madini hayo ni Kata za Kisiwani, Gonja, Ruvu na Same.

Kutokana na kugunduliwa kwa madini hayo, Senyamule ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo, ameagiza wachimbaji wote wadogo wanaofanya kazi hiyo wawe wamerasimishwa ndani ya siku 30.

“Naelekeza sasa, ofisa madini na timu yako, endeleeni na zoezi la kurasimisha maeneo yote ya uchimbaji wa madini yaliyopo ndani ya wilaya hii ili wachimbaji wachimbe madini kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazoongoza biashara ya madini. Hata hivyo, nawapongeza kwa kuleta madini sokoni na ninawahakikishia madini yaliyopo wanunuzi watakuja na kipato chenu kitaongezeka,” alieleza zaidi.

Alisema wilaya hiyo inayo hazina kubwa ya madini ambayo yameshagundulika na kuanza kuchimbwa na kwamba kuwepo kwa soko la madini katika Wilaya ya Same kumeongeza uhakika wa soko kwa wachimbaji wa madini ya vito na metali.

Hata hivyo, kuwapo kwa utajiri huo wa vito ni tofauti na matarajio kwamba eneo hilo lingekuwa na miundombinu mizuri ya barabara, upatikanaji wa huduma za kijamii na kukua kwa uchumi kwa eneo hilo kutokana na kuwa na madini adimu, lakini wilaya hiyo iko nyuma kiuchumi.

Katika kata hizo za Kisiwani, Gonja, Ruvu na Same, hakuna uwezekezaji mkubwa uliofanywa na watu binafsi katika migodi, huku barabara za kuingia na kutoka kata hizo zikiwa na vumbi, licha ya kuwa halmashauri tangu mwaka 1984.


Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, inawataka wachimbaji kuwa na leseni za uchimbaji ambazo zinatolewa na Wizara ya Madini na hutakiwa kupelekwa kwenye halmashauri husika kwa ajili ya kutoa taarifa na kuendelea na uchimbaji.

Habari Kubwa