Uanzishwe mfuko maalumu ili kuokoa zao la pamba, mengine

03Sep 2019
Raphael Kibiriti
DAR ES SALAAM
Nipashe
Uanzishwe mfuko maalumu ili kuokoa zao la pamba, mengine

DHAMIRA ya serikali kuwakwamua wakulima na hasa wadogo wadogo ambao ndio wanaunda sehemu kubwa ya Watanzania kwa maana ya shughuli kuu ya kiuchumi, ni ya msingi katika dhana nzima ya kujenga ustawi wao.

Serikali imefanya mengi ikiwamo hatua ya kuyatangaza baadhi ya mazao kuwa ya kimkakati kama vile pamba, korosho, kahawa, tumbaku na chai ili kuboresha  maslahi ya wakulima.

Na ndiyo maana kunashuhudiwa ongezeko katika uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini, ikiwa ni hatua stahiki kwenye mwelekeo wa kujenga utajirisho kwa wananchi.

Utajirisho ambao kwa mujibu wa Rais Yoweri Museveni alipomtembelea Rais John Magufuli, Chato Julai mwaka huu, unapaswa kuwa lengo namba moja la kila raia ili ajiletee maendeleo yake binafsi na hivyo taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, dhamira hiyo ya serikali ya kuona wakulima wananufaika na juhudi na uwekezaji wao katika kilimo inaonekana kukumbana na tatizo la soko la mazao yao.

Muungwana anachukua somo lililopatikana kwenye sakata la bei ya korosho na mazongezonge yake hadi pale serikali ilipoamua kununua korosho yote kama msingi wa anachokijadili.

Hiyo ni baada ya kampuni za ununuzi kugomea bei elekezi ya kuanzia Sh. 3000 kwa kilo iliyokuwa imewekwa na serikali, zikitaka kununua korosho kwa bei chini ya hiyo.

Aidha, kama haitoshi, kadhia hiyo imehamia pia kwenye zao la pamba ambako ununuzi wake kutoka kwa kampuni za ununuzi unasuasua hadi sasa pamoja na jitihada za serikali za kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao.

Kwamba pamoja na msimu wa pamba kuzinduliwa tangu mwezi Mei, hadi sasa bado pamba imejaa kwenye baadhi ya Maghala ya Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS), huku baadhi ya wakulima hasa katika Kanda ya Ziwa, wakiwa bado hawajalipwa fedha zao.

Na ndiyo maana kuna taarifa kwa mfano wiki iliyopita ya baadhi ya wakulima mkoani Shinyanga kufika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wakitaka kulipwa fedha zao, baada ya kuwa wameuza pamba yao.

Aidha, taarifa kutoka mkoani Simiyu, zinabainisha kwamba katika baadhi ya wilaya ikiwamo ya Maswa, kuna kama ‘kamgomo’ kutoka kwa wanunuzi wa zao hilo.

Kwamba wanataka kwanza waisafirishe pamba kutoka kwenye maghala ya AMCOS kwenda katika viwanda vyao, ndipo walete fedha kufuatana na kiasi cha kilo walichokisafirisha, kinyume na msimamo wa serikali.

Kwamba serikali inataka wakulima wakishauza pamba yao walipwe palepale na si kukopeshwa kama ‘matajiri’ wanavyotaka.

Matokeo yake mpaka sasa bado baadhi ya maghala ya AMCOS kwa mfano katika Wilaya ya Maswa yamejaa pamba, huku wakulima wakiwa bado hawajalipwa.

Hilo linafanyika mwezi Septemba tayari ukiwa umeshaingia, ambao kimsingi huwa ni wa kumalizia maandalizi ya mashamba kwa ajili ya msimu ujao.

Kadhia hii si kwamba inaathiri mwenendo mzima wa maandalizi ya msimu ujao, lakini dhana nzima ya utajirisho kwa mwananchi binafsi kama alivyoibainisha Rais Museveni kwenye ziara yake Chato ya kutaka kila mwananchi ajiletee maendeleo yake binafsi.

Maendeleo yatakayosaidia kuanzisha miradi binafsi kama ya ujenzi wa nyumba, hoteli, kupanua mashamba, mifugo na hivyo kukuza ajira na ustawi wa taifa.

Wakati Muungwana akiwahimiza wakuu wa mikoa na wilaya na hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kutoa uongozi utakaohakikisha wakulima wanalipwa fedha zao, ana ushauri kwa serikali.

Kwamba wakati umefika sasa wa kuwa na mfuko maalumu utakaokuwa mkombozi kwa wakulima pale kampuni binafsi za ununuzi zinapoleta ‘kamgomo’ kama inavyoendelea sasa kwenye zao la pamba au ilivyotokea katika zao la korosho.

Anasema hilo ni la msingi kwa sababu kutokana na somo lililoletwa na kadhia za ununuzi wa mazao hao mawili, kutegemea wanunuzi binafsi kunakwamisha dhamira njema ya serikali ya kuwajengea utajirisho wakulima.

Habari Kubwa