Taifa Stars morali juu wakiifuata Burundi

03Sep 2019
Shufaa Lyimo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Taifa Stars morali juu wakiifuata Burundi

TIMU ya Taifa ya Tanzania, 'Taifa Stars'  imeondoka leo alfajiri kuelekea Burundi tayari kwa mechi yao ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar 2022, itakayopigwa kesho nchini humo huku ikiwa na matumaini kibao ya kuibuka na ushindi.

Stars itatua Burundi ikitarajiwa kupokewa na waandishi wa habari za michezo kutoka vyombo mbalimbali pamoja na Kundi la Stars Sapoti, waliotangulia mapema kwa ajili ya kwenda kutoa hamasa nchini humo ili kuhakikisha Taifa Stars inashinda ugenini na kisha nyumbani.

Akizungumza na Nipashe jana asubuhi baada ya kumaliza mazoezi ya mwisho, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Juma Mgunda, alisema wachezaji wote morali yao ipo juu na lengo lao ni kuhakikisha wanarudi na matokeo mazuri.

“Leo tumefanya mazoezi ya mwisho, Mungu akipenda kesho alfajiri (leo) tutaondoka kuelekea Burundi ili tuwahi kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi ambapo tutakutana na wachezaji wetu wa kimataifa ambao tayari wapo Burundi wanaendelea kujifua,” alisema Mgunda.

Kocha huyo alisema wanaupa umuhimu mkubwa mchezo huo na kuwataka Watanzania kuiombea timu yao ifanye vizuri na kuipeperusha vema bendera ya Taifa letu.

Baada ya mechi hiyo, timu hizo zitarudiana Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, na mshindi wa jumla atasonga mbele kwenye hatua inayofuata.

Habari Kubwa