SUA inusuru upotevu huu

03Sep 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
SUA inusuru upotevu huu

SUALA la njaa na ukosefu wa uhakika wa chakula ni tatizo linalowapasua vichwa watu wengi lakini pia ni usumbufu kwa serikali.

Pamoja na kilimo cha Tanzania kwa kiasi kikubwa kutegemea mvua wakulima wanajitahidi kulima na wakati mwingine mazao mengi na kuifanya nchi kuwa na  ziada ya chakula.

Hata hivyo, habari njema hizo, zinakwazwa na upotevu wa chakula baada ya kuvuna na eneo linalotajwa kuwa limeathirika zaidi ni la nafaka.

Mazao yanayopotea kwa wingi baada ya kuvunwa kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ni pamoja na mahindi, mchele na mtama.

Ndiye anayedokeza kuwa kiwango cha upotevu wa nafaka baada ya mavuno ni asilimia 40.

Pamoja na maelezo yake, kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na  Chakula (FAO), wakulima nchini hupoteza hadi asilimia 40 baada ya mavuno kutokana na changamoto kama mtaji mdogo, ujuzi mdogo wa ubebaji mazao na ukosefu wa masoko na sera bora.

Utafiti mwingine wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine , unaeleza kuwa pamoja na ongezeko la uzalishaji katika ngazi ya kitaifa linalokadiriwa kufikia wastani wa tani milioni 9.4 kwa mwaka, teknolojia zinazotumika kabla, wakati na baada ya kuvuna husababisha upotevu wa wastani wa tani milioni 3.7 kwa mwaka sawa na asilimia 40.

Hata hivyo kuna tatizo jingine la mazao kuliwa na wanyama waharibifu yakiwa shambani, kwa mfano panya.

Si hao pekee, wakati mwingine kuna wadudu waharibifu kama dumuzi, vipepeo na bungua wanayoyaharibu, hata mchwa nao umekuwa ni tatizo kubwa hasa kwenye mahindi.

Licha ya wakulima kupambana na changamoto hizo kwa miaka mingi, mvua kunyesha baada ya mazao kukomaa yakiwa shambani nalo ni tatizo linalochangia upotevu wa chakula. Wakulima wengi huumizwa na mvua zinazonyesha wakati mahindi yakishakauka.

Aidha, baada ya mpunga kukomaa pia mvua hunyesha yote hayo huibua matatizo kama nafaka kuota, kuoza, kushambuliwa na mchwa na  pia kuvunda kutokana na kuvu wanaoibuka kutokana na unyevunyevu. 

Pamoja na utafiti huo wa SUA umefika wakati wa chuo kufanya kila jitihada kuwasaidia wakulima kuokoa mazao yao.

Hii ni kwa sababu taasisi hiyo ya umma pamoja na kupewa jukumu la kufunza wataalamu wa kilimo, mifugo na sekta nzima ya kilimo na ufugaji, uvuvi haitalitendea haki taifa iwapo kiwango kikubwa hicho cha chakula kitaachwa kupotea bila kunusuriwa.

Pengine  taasisi hiyo inaweza kujitetea kuwa haina fedha au bajeti ya kuzuia hasara hiyo lakini wakati umefika kwa Chuo Kikuu cha Kilimo kuwa mwokozi kwenye janga hilo.

Ni vyema kama ilivyofanya utafiti na kuibua asilimia za upotevu, ikachunguza pia na kuanzisha program na miradi ya kuwasaidia wakulima kulinda mazao baada ya mavuno.

Licha ya kutafiti na kuibua changamoto hizo

wananchi wanaweza kuendelea kupata hasara kama hakutakuwa na msaada wa kudhibiti upotevu wakulima wataendelea kuumia.

Tungependa kuona SUA ikianzisha program za jinsi ya kuhifadhi nafaka pengine ikihusisha kujenga vihenge vya muda kwani suala la utunzaji duni mazao husababisha kupoteza chakula kingi.

Aidha, chuo kiangalie namna ya  kuwafunza wakulima namna bora za kuchakata mazao mara moja baada ya kuvuna kuzuia yasiharibikie mashambani.

Halikadhalika kuwasaidia  kubuni mbinu bora za kuyasafirisha ili kuzuia upotevu wa chakula unaotokea sehemu mbalimbali ambao pengine kiasi uzalishaji unavyopanda nao unaongezeka pia.

Habari Kubwa