Taharuki yaibuka basi la mwendokasi likiteketea

03Sep 2019
Beatrice Moses
DAR ES SALAAM
Nipashe
Taharuki yaibuka basi la mwendokasi likiteketea

 TAHARUKI iliwakumba baadhi ya abiria wa mabasi ya mwendokasi, baada ya basi moja  kuwaka moto na kuteketea wakati likiingia kwenye kituo cha Kimara jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo limetokea juzi usiku,  licha ya dereva  wa basi hilo kufanikiwa kuwanusuru abiria na yeye mwenyewe, abiria waliokuwa kwenye mabasi mengine walitawaliwa na hofu kuwa miali ya moto huo  kuwa unaweza kulipua magari mengine. 

Baadhi ya abiria walitamani kuruka kupitia kwenye madirisha ili kunusuru maisha yao, baada ya kuona madereva wanajishauri  kuhusu kufungua milango ili washuke kwa kuwa hapakuwa mahali sahihi na salama kushusha.  

Kamanda wa Kikosi za Zimamoto na Uokoaji Kinondoni, Jenifer Shirima, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo akibainisha kuwa  ni jambo la kushukuru kuwa hakuna binadamu  aliyejeruhiwa ama kusababishiwa kifo na moto huo.

“Tulipokea taarifa ya kuzuka kwa moto huo saa 2:03. Mtambo wetu uliwasili eneo la tukio saa 2:15  ukiwa na maji lita 8,000 na kufanikiwa kuzima moto huo,” alisema Kamanda Shirima.

Alibainisha kuwa taarifa za awali zinabainisha kuwa chanzo cha moto huo kilikuwa ni uvujaji wa mafuta ambao ulibainika gari likiwa katika eneo la Baruti, dereva aliwahakikishia kuwa watafika salama Kimara.

“Msuguano unaosababisha joto unapokutana na petroli kwa kuwa ni hewa ina uwezo wa kusababisha moto kuwaka, ndicho kilichotokea lilipokaribia kituoni basi lilianza kuwaka moto,” alisema Kamanda Shirima.

Alisema uchunguzi zaidi unaendelea kufanywa  kujiridhisha na chanzo cha moto huo kisha watatoa taarifa rasmi.

“ Nawasihi wananchi wajitahidi kuhakikisha wanatoa taarifa haraka iwezekanavyo kwa kupiga namba 114 mara moto unapozuka, kisha ndipo waendelee na juhudi za kuzima, kwa tukio hilo tulifika kwa wakati kulingana na muda tuliopata taarifa,” alisema.

Alisema basi hilo lilitoka mjini likiwa na abiria na lilipofika eneo la Kimara Mwisho walifanikiwa kushuka kabla halijateketea kwa moto.

Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na kukusanya taarifa zaidi za ajali hiyo, ikiwamo hasara iliyosababishwa na ajali hiyo.

Tukio hili si la kwanza kwa basi la Udart kuwaka moto kwani huko nyuma eneo la Ubungo Dar es Salaam liliwahi  kutokea ila uliwahi kudhibitiwa.

Habari Kubwa