Kigogo adaiwa kukwepa kodi kontena 700

03Sep 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kigogo adaiwa kukwepa kodi kontena 700
  • *Amfuata JPM kuomba huruma…

KATIBU wa Itikadi na Uenezi Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, amedai kuwapo kwa kiongozi mmoja mkubwa nchini anayedaiwa kuingiza mzigo wa kontena 700 bandarini.

KATIBU wa Itikadi na Uenezi Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole.

Alidai kuwa kiongozi huyo alitaka kukwepa kodi ya kontena hizo kwa kutaka huruma ya Rais John Magufuli.

Polepole alitoa madai hayo mwishoni mwa wiki katika kongamano la umuhimu wa amani na mapambano dhidi ya rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, mwakani.

Kongamano hilo liliandaliwa na Jumuiya Waislamu wa Shia Tanzania na kuhudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa tawala na upinzani, viongozi wa dini na wadau mbalimbali.

Akifafanua kuhusu kiongozi huyo, Polepole alisema; "yupo kiongozi mmoja mkubwa sana Tanzania sitamsema hata Takukuru wanamfahamu, ila mniwie radhi sitamtaja jina, alikuwa na kontena 700 bandarini amekwepa kodi.

"Kila kontena moja lilikuwa na futi 40, huyu kiongozi alitaka Rais amsaidie, lakini Rais Magufuli alimwambia lipa kodi uende zako. Huyu kiongozi mpaka sasa amenuna," alidai.

"Hivi ninavyoongea mpaka sasa amenuna. Rais Magufuli kazi yake ni kushughulika na watu walionuna. Siku zote ukisimamia haki hupendwi. Mtume alisimamia haki hakupendwa, Yesu alisimamia haki Wayahudi wakamuua, Ayubu alisimamia haki akapoteza kila kitu hadi familia yake."

Alidai kuwa hakuna mtu anayesimamia haki na akaishi maisha ya starehe bali huishi kwa imani.

"Rais Magufuli anatekeleza miradi ya maendeleo, lakini wapo ambao bado wanasimama wanasema hafanyi kitu, amenunua ndege wapo waliobeza, ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalisha umeme, wapo waliopinga kwa kusema uharibifu wa mazingira.”

"Rais Magufuli ndiye pekee ambaye ameweza kutumia fedha za ndani na huu ndio ugomvi mkubwa uliopo na wao, miradi ya kimkakati inayotekelezwa ni kwa fedha za walipa kodi."

Alisema tangu mwaka 1961 hadi awamu ya nne vituo vya afya ambavyo vilijengwa vilikuwa ni 115, lakini kwa miaka miwili kuanzia mwaka 2017 Rais Magufuli amefanikiwa kuvijenga vituo 350.

"Hospitali zilizojengwa kwa awamu zilizopita zilikuwa 77, lakini kuanzia mwaka 2018/19 Rais Magufuli amejenga hospitali 67, zimebaki 10. Wapo waliokuwa wanatamani kuona korosho zinakwama, leo zinasombwa Mtwara malori kwa malori," alisema.

Pia, alisema serikali ilimkamata jambazi mmoja akiwa amejificha kwenye moja ya makabati Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, akiwa anajiandaa kutoroka nchini.

"Amejificha kwenye makabati kwenye maduka pale uwanja wa ndege, cha ajabu hakuonekana kwenye kamera yoyote uwanjani hapo namna alivyoingia kwenye makabati hayo, alikuwa anasubiria tangazo la kuingia kwenye ndege aliyokuwa akisafiri nayo ili akishaingia tushindwe kumkamata, lakini intelijensia yetu ilimkamata na sasa hivi yupo Segerea," alidai.

"Naipongeza Shia kwa kuandaa kongamano hili ambalo limetukutanisha wanasiasa na viongozi wa dini ili tuzungumze, nawaomba makongamano kama haya muwe mnayaandaa kila mara," alisema.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Msafiri Mtemelwa, alipopewa nafasi ya kuzungumza alilalamika kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara na vikao vya ndani.

Hata hivyo, akijibu hoja hiyo Polepole alisema siyo kweli kwamba vikao vya ndani vimezuiliwa na kutoa mfano wa majimbo mawili ya upinzani la Arusha na Mbeya Mjini ambako kote wanavifanya.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ally Mfuru, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wake, alisema taasisi hiyo inajipanga vyema kuhakikisha wanafanya kampeni kuanzia chini ili kuwakumbusha wananchi kutojihusisha na rushwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuelekea Uchaguzi Mkuu, mwakani.

Mhadhiri katika chuo cha Swadiq chini ya kiongozi Mkuu Maulana Sh Hamed Jalala, Saidy Othman, aliiomba serikali ili kutengeneza fikra na mitazamo mipya somo la rushwa lifundishwe shuleni wanafunzi waanze kujua ubaya wake tangu wakiwa wadogo.

Alisema vitendo vya kubaka, dhuluma na kula rushwa vyote vinafanywa na binadamu bila kushirikisha akili.

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Dk. Mohamed Ahmed, alisema, yeyote atakayejaribu au mwenye mawazo ya kusababisha matatizo hatakuwa na nafasi Tanzania.

Habari Kubwa