Yanga yafunguka kutimuliwa Zahera

03Sep 2019
Shufaa Lyimo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga yafunguka kutimuliwa Zahera
  • ***Sababu kuitwa kwenye kikao zaanikwa, huku suala la kutua kwa Mserbia kuinoa nalo likielezwa...

WAKATI taarifa zikizidi kuzagaa huku baadhi ya vyombo vya habari (si Nipashe) vikiripoti kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amekalia kuti kavu na kwamba amepewa mechi tatu za kushinda vinginevyo atatimuliwa, uongozi wa Yanga umefunguka A-Z kuhusu sakata hilo.

Awali chanzo chetu ndani ya klabu hiyo, wakati tukitafuta ukweli kuhusu sakata hilo, kililiambia Nipashe kuna taarifa za kuanza kutafutwa kocha Mserbia atakayeinoa klabu hiyo kutokana na mwenendo wa timu kufanya vibaya licha ya Zahera kusimamia suala zima la usajili.

"Lakini pia uongozi hakufurahishwa na kocha kuukosoa hadharani licha ya baadhi ya mambo kukubaliana nao ikiwa ni pamoja na kupendekeza kambi iwekwe mikoa ya Kaskazini ili wachezaji wazoee hali ya baridi kabla ya kwenda kurudiana na Township Rollers ya Botswana kwenye Ligi ya Mabingwa," kilieleza.

Hata hivyo, Nipashe lilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela, ambapo alikanusha vikali taarifa hizo kwa kueleza kwamba si kweli kuwa kocha Zahera amepewa mechi tatu za kuhakikisha anashinda bali juzi kulikuwa na kikao cha Kamati ya Utendaji na kocha aliitwa ili kutambulishwa rasmi kwa wajumbe na pia kutoa mikakati ya kuelekea mechi dhidi ya Zesco Septemba 14, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mwakalebela alisema kwa ujumla uongozi una imani na kocha huyo na wana ushirikiano mzuri hivyo habari kwamba amepewa mechi tatu zipuuze vikali.

Mwakalebela alisema habari hizo hazina ukweli wowote na badala yake zinasambazwa na watu wachache ambao hawaitakii mema timu yao.

“Hizo habari za kwamba tunaachana na Mwinyi Zahera si kweli tunamtambua Zahera kuwa mpaka sasa ndiye kocha wetu mkuu hakuna kitu kama hicho hayo ni maneno ya uzushi sasa hivi tunajiandaa na mchezo wetu dhidi ya Zesco United,” alisema Mwakalebela.

Aidha, alisema timu yao inatarajiwa kuelekea mkoani Mwanza kesho kwa ajili ya kuweka kambi mpaka Septemba 11, mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kucheza mechi za kirafiki ambazo zitakuwa ni mwendelezo wa maandalizi ya mchezo wao huo dhidi ya Zesco.

“Timu yetu inaendelea na mazoezi kama kawaida tukiwa tunajiandaa na safari yetu ya Mwanza ambapo tutakwenda kuweka kambi na kucheza michezo ya kirafiki tunaomba Watanzania wazidi kutupa ushirikiano katika mchezo huo ili tuweze kuipeperusha vema bendera ya Taifa,” alisema.

Kwa upande wa leseni za wachezaji wao ambao hawakucheza mchezo wa raundi ya kwanza, alisema bado hazijafika na kwamba wanaendelea kuzifuatilia na kudai endapo zikiwa tayari Watanzania watajulishwa.

Habari Kubwa