Ziwa Manyara hatarini kutoweka

04Sep 2019
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
Ziwa Manyara hatarini kutoweka

HIFADHI ya Ziwa Manyara mkoani Arusha, iko hatarini kutoweka baada ya  kujaa matope, kutokana na wakulima na wafugaji wanaolizunguka kufanya shughuli zinazoingiza matope na taka ziwani.

Wakulima na wafugaji wanalima na kufuga   pembezoni mwa ziwa hilo, na kusababisha udongo kuingia kwa wingi na kuchafua ziwa.

Hayo yalisemwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Hifadhi ya Manyara, Noelia Myonga, wakati akitoa taarifa ya hifadhi ya ziwa hilo, kwa wataalamu na wanasayansi wa mazingira waliotembelea hifadhi hiyo, kwa lengo la kuangalia changamoto zinazoikabili.

Myonga alisema, wanakijiji wanaozunguka ziwa hilo, wanaofanya shughuli za kilimo zisizokuwa endelevu na  wamesababisha kina cha ziwa hilo kuwa kifupi zaidi na maji kupungua.

Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa wizara zinazohusika kuchukua hatua ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umuhimu wa ziwa hilo kuendelea kuwapo.

Alisema hifadhi hiyo, kwa kushirikina na Shirika la Hifadhi za Taifa wametoa elimu ya matumizi bora ya ardhi kwa vijiji 25, ili kuwepo na matumizi sahihi ya ufugaji na kilimo chenye tija ambapo itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira ndani ya hifadhi hiyo.

Ofisa Mazingira wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Fredrik Mulimba, alisema baada ya kufanya ziara hiyo, wamebaini kuwa maji yanapungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Aidha, alisema mamlaka husika inatakiwa kuwekeza nguvu nyingi katika hatua ya kutatua tatizo hizo kwa muda mwafaka ili kuilinda hifadhi hiyo, viumbe hai na wanyamapori wanaoishi katika eneo hilo.

“Kutokana na changamoto zinazoikabili hifadhi ya ziwa serikali inapaswa kuchukua hatua  ili kulinda Hifadhi ya Ziwa Manyara na viumbe hai na wanyamapori wanaoishi katika eneo hilo,” alisema Mulimba.

Habari Kubwa