Aeleza umuhimu wa kujua mambo ya kale

04Sep 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Aeleza umuhimu wa kujua mambo ya kale

WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo, amesema Wazanzibari wanahitaji kujua mambo mengi ya kale ili waweza kufahamu historia ya nchi yao.

WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya jengo la kihistoria la Bi Hole lililoko huko Bungi baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa, alisema hali ya jengo hilo hivi sasa ni ya ubora wa hali ya juu na  amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kutembelea sehemu za historia.

Maeneo hayo ni kama Bi Hole, Dunga, Mkandamume, Fukuchani na Mvuleni ili kuendeleza utalii wa ndani.

 

Alisema lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka idara maalum inayoshughulika Mambo ya Kale ni moja ya njia ya kuwekeza na kukuza uchumi hasa ukizingatiwa kwamba Zanzibar ina utajiri mkubwa wa mambo ya kale.

 

Aidha, alisema sehemu hiyo itakapokamilika itakuwa na uwezo mkubwa wa kupokea wageni na wenyeji watakaotembelea na kutakuwa kuna mvuto kama ilivyo kwa Forodhani  na  Fumba.

“Eneo hilo likikamilika linatarajiwa kuwa na mambo mengi yaliyo mazuri ikiwamo sehemu ya kupumzikia, biashara za vyakula,  burudani ili kuweka mazingira bora  pahala hapo,” alisema Waziri Kombo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Mambo ya Kale, Khadija Bakari, alisema serikali inafanya  juhudi kubwa kwa makusudi ili kuimarisha majengo ya mambo ya kale na kuwa vivutio vya kukuza utalii.

Hivyo aliwaomba watakaokuwa wanashughulikia jengo hilo kuhakikisha wanaweka ulinzi ulio imara ili jengo hilo lisichafuliwe na liweze kudumu kwa muda mrefu.

“Nawaomba walinzi kuwa imara na kuhakikisha jengo hili isiwe watu wanaingia na kutoka na lisichafuliwe kwa makusudi ili liendelee kupendeza pia liweze kufanya kazi kwa muda mrefu,” alisema Katibu huyo.

Kwa upande wake mhandisi wa kampuni ya Azim iliyojenga jengo hilo Abdullah Omar alisema ujenzi huo umeanza mwaka mmoja uliopita na mambo yote waliyokubaliyana kwenye mkataba yamemalizika.

Mradi huo wa jengo la Bi Hole hadi kukamilika umegharimu Sh. milioni 800 ambazo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Habari Kubwa