Afrika yaonywa itakabwa na mkate, siagi kutoka China

04Sep 2019
Gaudensia Mngumi
DAR ES SALAAM
Nipashe
Afrika yaonywa itakabwa na mkate, siagi kutoka China

MKUTANO wa Mataifa ya Afrika na Japan, uliomalizika Japan wiki iliyopita haujainyamazia China kuhusu ushirikiano na Afrika ambao unaacha mzigo wa madeni.

Mkutano huo maarufu kama Tokyo International Conference on African Development (TICAD), unasimamiwa na Serikali ya Japan kuanzia mwaka 1993, ukishirikisha wadau kama Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Benki ya Dunia (WB) na Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Afrika (AUC).

Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, amewaambia viongozi wa Afrika wagutuke kuhusu deni la China na kuchukua tahadhari kwenye ushirika na taifa hilo ambao kwa mujibu wa madai yake unawaingiza Waafrika hatarini.

Abe, anaonya dhidi ya kuzibebesha madeni makubwa nchi za Afrika, akisema wawekezaji katika bara la Afrika hawana budi kuwa na tahadhari dhidi ya kuzitwika mzigo mkubwa wa madeni nchi hizo zenye uchumi unaokua na watu maskini, japo bara lao limejaa rasilimali za kutosha.

Japo Abe anaonekana kuelekeza  zaidi ujumbe huo kwa China, ambayo sera yake ya ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara imekuwa ikikosolewa kwamba inaziangamiza nchi maskini kwa kuzibebesha madeni makubwa, angalizo lake ni muhimu.

Kiongozi huyo akizungumza baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa ushirikiano jijini Tokyo, anasisitiza kwamba nchi za kundi la mataifa yenye uchumi mkubwa duniani za G20 ikiwamo China zimejitolea.

Ni katika mpango wa kuyadhibiti madeni ili kuiepusha Afrika na mzigo mkubwa inayoubeba, jambo linalopaswa kuzingatiwa ili  yasipite kiwango cha uwezo wa Afrika.

Baadhi ya miradi ya reli ambayo anaizungumzia Abe ni kama ile iliyoko Nigeria, Angola na Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Habari la China- Xinhua, China imejenga na inaendelea kukamilisha ujenzi wa reli za kisasa za (SGR) kutoka Mombasa hadi Nairobi nchini Kenya na ya Addis Ababa Ethiopia hadi nchi jirani ya Djibouti.

Xinhua linasema mwaka 2015, China ilikamilisha ujenzi wa kilometa 1,344 za reli ya kisasa nchini Angola, iliyounga miji ya pwani ikianzia Lobito hadi jiji la Luau lililoko mpakani na Congo.

Hii ni reli ndefu Afrika iliyojengwa na kampuni ya China ikiwa ni ya pili baada ya TAZARA. Reli hiyo inaunga miji mikuu na majiji ya Angola, Zambia, Tanzania na Congo pia.

Aidha, China imejenga SGR kutoka Abuja hadi jiji la Kaskazini la Kaduna nchini Nigeria, ikiwa na kilometa 187, kazi iliyokamilika mwaka 2016 kwa mujibu wa Xinhua.

 

Nigeria imeendelea kunufaika na China kwenye ujenzi wa reli nyingine ya kisasa inayounga majiji ya Lagos na Ibadan na kwa ujumla China inashirikiana na Umoja wa Afrika (AU), kujenga reli ya kisasa itakayounga miji mikuu ya bara hili.

Miaka miwili iliyopita katika moja ya mikutano yake na wakuu wa serikali za Afrika, ilitangaza mpango wa kutoa Dola bilioni 60 (zaidi ya trilioni 130) kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Afrika.

AU MAKAO MAKUU

Sekretariati na Ofisi za Umoja wa Afrika, vituo vya mikutano na kwa ujumla makao makuu ya AU yaliyoko Addis Ababa nchini Ethiopia maarufu kama (AUCC), ni kazi iliyofanywa na China.

Lakini, pembeni ya makao hayo makuu ndiko yaliko makao makuu ya Shirika la Misaada la China la China-Aid.

Gharama za ujenzi huo zilizoko kwenye mtandao zinaonyesha kuwa ilitumia zaidi ya Dola milioni 200 sawa na bilioni 460 kujenga makao ya AU.

 

UMEME WA INGA

China pamoja na AU zina ubia wa ujenzi wa bwawa la umeme la Grand Inga, lililoko kwenye Mto Inga nchini Congo.

Maporomoko yaliyoko ndani ya Mto Inga yanatarajiwa kuzalisha takribani megawati 40,000 za umeme zitakazolisha umeme Afrika nzima na kupunguza tatizo la nishati hiyo.

 

KUOGOPA MADENI

Kwa hiyo, akiangalia mambo mengi yanayotumia mabilioni ya dola, Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, anawaambia viongozi wa Afrika wawe macho na kujilimbikizia madeni kutokana na mikopo na kandarasi nyingi za miundombinu ya kisasa inayofanywa na China, kwa vile mambo yatawaangukia na kuwaumiza.

Katika mkutano wa Yokohama, Abe anahoji nini kifanyike na anaahidi kuwa Japan katika miaka mitatu ijayo inatarajia kufunza wataalamu 30 wa Afrika kufahamu jinsi ya kukabiliana na hatari ya madeni ya umma.

 

Hata hivyo, angalizo la Abe linaikumbusha Afrika mambo mengi.

AFRIKA IFANYEJE ?

Afrika lazima itambue vipaumbele vyake, iwekeze itekeleze majukumu yake na si lazima kufuata utaratibu wa maendeleo unaofanyika Ulaya na Marekani.

Ni lazima ijiondoe kwenye utegemezi wa nchi za Magharibi, AU ijizatiti kwenye kusimamia na kuendeleza ushirikiano wa kikanda ili kuwa na mtangamano unaokuzwa na ushirika  wa kikanda.

Afrika iwekeze kwenye ushirikiano wa kibiashara, ushindani wa viwanda, kilimo na kuimarisha miundombinu yake kwa utaratibu unaolifaa bara hilo na si kuigiza.

Bara la Afrika lifanikishe kuanzishwa kwa ukanda huru wa kibiashara ‘Free Trade Area’ na mataifa yote 54 yashiriki kwenye mtangamano huo wa kibiashara na kiuchumi badala ya kutegemea biashara na  China, Umoja wa Ulaya na mipango kama ule wa Marekani wa AGOA, ambao si vitu endelevu.

Waziri Mkuu Shinzo Abe, anamaanisha kuwa hatma ya Afrika iko mikononi mwa viongozi wa bara hilo tajiri japo maskini. Ni lazima viongozi wajue kufanya mikataba ya kibiashara ya ‘kijanja’  wasikubali kutapeliwa na wajihusihe kwenye uwekezaji wa tija na siyo kukubali ili wapate kile wanachohitaji kwa wakati huo bila kujali athari za baadaye.

Wakitaka SGR leo, miradi mikubwa ya umeme kama wa Inga na barabara za kisasa wajue kuwa leo ni kukopa harusi lakini kesho kulipa ni matanga.

Si kwamba anawapenda sana Waafrika kila mmoja hapa anaangalia maslahi yake. Japan kupitia mkutano wa TICAD kila mwaka inaangalia namna ya kuendeleza maslahi yake na ushirikiano na Afrika.

Wakati china ina shirika la ukandarasi la China Railway Construction Corporation Limited (CRCC) linalojenga reli kila mahali, Japan nayo ina Konoike na Kajima.

Kwa ujumla Afrika ijitegemee isimame yenyewe kama ina watu bilioni moja ni soko la kutosha. Izingatie mikataba yake kama ule wa Demokrasia, Uchaguzi na Uongozi (ACDEG) ,ambao ni dira inayoielekeza Afrika cha kufanya ili ifikie maendeleo ya kweli na endelevu.

Hofu ya Japan ni kwamba pengine itafika kipindi Congo na AU ikashindwa kuendesha mradi wa umeme wa Inga kulipa deni hapo , italazimika kaacha jukumu hilo kwa China isimamie uendeshaji ili kulipa fedha zake.

Aidha, Kenya na Ethiopia zikishindwa kulipa deni la ujenzi wa SGR, Serikali ya Beijing italazimika kuichukua ili kujilipa madeni yake.

Yote hayo yatahatarisha ‘sovereignty’ ambayo ni haki ya kila taifa kuwa huru kujiamulia mambo yake bila kuingiliwa na yeyote.

Habari Kubwa