DC Muwango: Nachingwea ni ya maendeleo kwanza, ndipo vyama

04Sep 2019
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
DC Muwango: Nachingwea ni ya maendeleo kwanza, ndipo vyama

MOJA ya mambo, ambayo Rais Dk. John Magufuli amekuwa akihimiza, ni watu kufanya kazi bila kubaguana kwa namna yoyote ile ikiwamo ya itikadi za vyama, kwa vile maendeleo hayana chama.

Rais anaamini kwamba viongozi huteuliwa kushika nafasi mbalimbali kutokana na uwezo wao wa utendaji kazi pamoja na uadilifu wao na pia wanatakiwa kuwasilikiza wananchi na kutatua matatizo yao.

Viongozi wanakumbushwa kuwa jukumu lao ni kusimamia kikamilifu shughuli mbalimbali za serikali zitakazochochea maendeleo ya wananchi kwa ngazi zote, wakitambua kuwa maendeleo hayana chama.

Anawashangaa baadhi ya watu wanaosema kuwa ameteua wapinzani, lakini anaamini kwamba kwa Tanzania anayoijenga ya umoja, vyama na ukabila vikitangulizwa, nchi haiwezi kufika mbali.

Kwa kuzingatia kauli hiyo ya mkuu wa nchi, wapo baadhi ya viongozi ambao wanaitekeleza kwa vitendo ili kuhakikisha wananchi kwenye maeneo yao wanafanya shughuli za maendeleo bila kubaguana kwa itikadi za vyama.

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango ni miongoni mwa viongozi hao, ambaye amejiwekea utaratibu wa kukutana na madiwani wa vyama vya upinzani na kuweka mikakati ya maendeleo.

Anasema upinzani wilayani mwake upo, lakini hauna nguvu sana, kwa vile unaongoza kata tisa kati ya 36.

Pamoja na ukweli huo, bado anashirikiana nao kwa vile maendeleo hayana chama.

Muwango anafafanua zaidi jinsi anavyoshirikisha upinzani kwenye shughuli za maendeleo wilayani mwake, katika mazungumzo aliyoyafanya na gazeti hili. Fuatilia mahojiano hayo:

SWALI: Unasema unashirikisha upinzani kwenye shughuli za maendeleo, unaushirikisha vipi?

JIBU: Kwanza kabisa nikuhakikishie kwamba upinzani wilayani kwetu unatambua kazi kubwa ya kuleta maendeleo inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na madiwani wa kata sita wakiwamo wa Chadema na CUF wanatoa ushirikiano mkubwa kwangu, kwani ninakutana nao na kupanga shughuli za maendeleo na wanazitekeleza vyema kwenye maeneo yao.

Kwa mfano, wanahamasisha ujenzi wa vyumba vya madarasa, zahanati na pia kituo cha afya cha Kata ya Namapwiya. Yaani kwa ujumla ni kwamba huku kwetu ni maendeleo kwanza vyama baadaye, kwa sababu nchi hii inajengwa na Watanzania wenyewe bila kujali itikadi za vyama vyao.

Na kwa kutambua hilo tunashirikiana vizuri tu kuijenga Nachingwea yetu. Binafsi kama mkuu wa wilaya sijapata ugumu wa kusimamia shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao, kwani ninatoa maagizo, wanatekeleza. Yaani wananipa ushirikiano mzuri tu kwa ajili ya maendeleo ya maeneo yao na Nachingwea kwa ujumla.

Ninapoitisha mikutano wanahudhuria kwa wingi na wanasaidia kuhimiza wananchi kuhudhuria mikutano yangu. Ni muhimu kila mmoja wetu atambue kuwa maendeleo ya kweli hayana chama, kwani shida za kimaisha hazibagui chama. Hivyo, hatuna budi kufanya kazi kwa pamoja kama Watanzania na si kwa sababu ya kuwa wanachama wa chama fulani.

SWALI: Unasema wapinzani wana kata tisa ni zipi hizo?

JIBU: Kata zinazoongozwa na upinzani ni Mpiruka, Marambo, Naipanga  (Chadema), Mkoka, Ndomoni, Kiegei, Chiola, Namapwia na Kipara Mnero  zote ziko chini ya Chama cha Wananchi (CUF). Kata zingine 27 ambazo ziko CCM ni Boma, Chiumbati Shuleni, Kilimani Hewa,  Kilimarondo, Kipara, Mtua, Lionja, Matekwe na  Mbondo. Zingine ni Mchonda, Mitumbati, Mkotokuyana,  Mnero Miembeni, Mnero Ngongo, Mutua, Nachingwea Mjini, Naipingo na Namatula.

Aidha kata za   Nambambo, Namikango, Nang'ondo, Nangowe, Nditi, Ngunichile, Raha leo, Ruponda, Stesheni na  Ugawaji. Hata hivyo, hatuwezi kudharau uwakilishi na mawazo yao yanayohusu maendeleo ya wilaya yetu. Sisi sote ni wana Nachingwea na kimsingi maendeleo hayana chama.

SWALI: Ni njia gani unazotumia kutatua kero za wananchi?

JIBU: Binafsi nimejiwekea utaratibu wa kukutana na wananchi Alhamisi ya kila mwisho mwezi nikiwa na wakuu wa idara zote na taasisi za Serikali kusikiliza kero zao, huwa ninakwenda kila tarafa. Hapa kwetu tuna tarafa tano za Kilimarondo, Naipanga, Nambambo, Lionja na Ruponda. Ninakutana nao kwenye tarafa ili kama kuna maelekezo nimeyatoa, basi viongozi wa tarafa washushe kwenye kata na wa kata washushe kwenye Serikali za Mitaa.

Lengo ni kuhakikisha wananchi wote wanapata taarifa au maelekezo kutoka kwa mkuu wao wa wilaya.

Lakini lengo la kutembea na wakuu wakuu wa idara na taasisi za Serikali ni kutaka kila mmoja ajibu kero za wananchi kama zitaelekezwa kwake na mwisho wa siku kama kuna tatizo basi linapatiwa ufumbuzi kama utakuwa ni wa hapo hapo au kusubiri.

Njia hiyo imesaidia kuwa karibu na wananchi, kwa kuzingatia kwamba kuongoza ni kuelekeza na pia siyo kukaa ofisini tu bali kufika kwa wananchi ili kusikiliza kero zao.

Siishii hapo tu bali pia pamoja na viongozi wenzangu wakiwamo wanasiasa wanafanya kazi ya kuelimisha wananchi kutambua umuhimu wa Daftari la Kudumu la Mpigakura ili hatimaye litakapofika hapa wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na hatimaye waweze kushiriki katika uchaguzi ujao.

Kazi hii ya kuhamasisha inafanywa na wanasiasa wa vyama vyote, kwani kama nilivyosema, maendeleo hayana chama... kuhamasisha wananchi kwa ajili ya kujiandikisha kwa lengo la kupiga kura ni hatua mojawapo ya kuwatambua viongozi watakaosimamia shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao.

SWALI: Kiutaratibu wewe ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani mwako. Je, hali ya usalama Nachingwea ikoje?

JIBU: Nachingwea ni shwari kabisa na suala la udokozi mdogo mdogo unaofanywa na baadhi ya vijana wasiotaka kufanya kazi siwezi kulichukulia kwamba linahatarisha usalama wetu.

Kwa hiyo Nachingwea ni shwari kabisa, askari wanafanya kazi vizuri kuhakikisha wakati wote watu wanakuwa salama. Lakini pamoja na usalama huo, hatuwezi kubweteka bali tunaendelea kuimarisha ulinzi, na ninakuhakikishia kuwa Nachingwea ni miongoni mwa wilaya ambazo hazina changamoto za vitendo vya uhalifu.

Kwa sababu kila ninapokutana na wananchi pamoja na mambo mengine, huwa siachi kuhimiza suala la usalama na wananchi katika maeneo yao wameunda vikundi ambavyo vinahakikisha wananchi wanaishi kwa amani.

Ikumbukwe kuwa shughuli za maendeleo haziwezi kufanyika iwapo hakutakuwa na usalama, hivyo kwetu usalama ni jambo la kwanza ndio maana tupo shwari.

Habari Kubwa