Hili la moto mwendokasi ni changamoto uokoaji

04Sep 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hili la moto mwendokasi ni changamoto uokoaji

KUUNGUA kwa basi la mwendo kasi juzi jijini Dar es Salaam kumeongeza hofu ya usalama ndani ya vyombo vya usafiri vya umma.

Woga unatokea kwa sababu hakuna usalama wa kutosha ndani ya vyombo vya usafiri wa umma licha ya kwamba ni  muhimu kuliko chochote kile kwa vile usafiri huo hubeba idadi kubwa au abiria wengi kupindukia.

Hali inakuwa mbaya zaidi kwenye magari ya mwendo kasi ambayo licha ya kuwa na abiria wengi sana hakuna mifumo madhubuti ya kuwahakikishia usalama na hata ya kufanikisha uokoaji pale tatizo linapotokea.

Changamoto kubwa ni kwamba watu wengi hawafahamu jinsi ya kujiokoa iwapo ajali itatokea mbali na kufikiria kuwa wanaweza kuruka dirishani.

Pamoja na kukosa ufahamu wa jinsi ya kujiokoa abiria wengi hawana wazo kuhusu usalama wao na wengi hupanda kwenye magari bila kujali kuwa chochote kinaweza kutokea hasa gari kuwaka moto nao wakashindwa kuokoka.

Watanzania wengi hawajali wala kuwaza iwapo ajali itatokea watajiokoaje? Ndiyo maana wanapoingia kwenye gari hakuna anayejishughulisha kutafuta jinsi ya kujiokoa kama ajali inatokea.

Hata hivyo, tusilaumiane bali kuanzia sasa serikali na mamlaka ziimarishe miundombinu na mifumo ya kujiokoa ndani ya mabasi ya umma.

Tukiwageukia wasafirishaji wa mwendokasi, pengine tuwahoji hivi wana utaratibu gani wa kujiokoa?

Kubwa ni kwamba milango ya gari za mwendokasi hufunguliwa kwa mfumo wa umeme kazi inayofanywa na injini, hivyo iwapo ajali itatokea kwa sababu za hitilafu kwenye injini itakuwa vigumu kufungua milango hiyo.

Na kama kuna ajali iliyokwamisha injini inamaanisha kuwa uwezekano wa milango kufunguka ni mdogo hivyo majeruhi na vifo vinaweza kuwa vingi sana.

Kwa hiyo kazi ya kwanza ambayo magari ya mwendokasi yanatakiwa kuipatia majibu ni hiyo ya milango ya kujiokolea.

Suala jingine ni jinsi ya kushuka kwenye magari hayo ambayo mara nyingi yanategemea ukingo wa barabara za ndani ya  vituo ili abiria kupanda na kutoka.

Swali letu ni hili , hivi iwapo tatizo litatokea nje ya kituo itakuwaje?  Jambo hili nalo walitafakari itakuwaje kama gari litapata hitilafu ya moto njiani na wala si ndani ya kituo?

Je inawezekana kwa mabasi ya mwendokasi kuwa na milango ya kuokolewa watu ambayo itafunguliwa kwa nguvu za binadamu badala ya hiyo inayojiendesha yenyewe?

Vipi magari haya yana ngazi za kuokolewa watu iwapo ajali itatokea katika eneo ambalo si kituoni?

Ni vyema kufikiria suala hilo kwani milango ya magari hayo hata kama inafunguka iko juu kiasi kwamba ni vigumu abiria kushuka chini kwa haraka ili kujiokoa ajali inapotokea.

Ni eneo la kuchukua tahadhari kwa kuwa abiria wanaweza kukanyagana na kuumizana iwapo hakutakuwa na udhibiti kwenye eneo la kutoka mlangoni.

Tatizo jingine la magari haya ni kukosa madirisha makubwa yanayowezesha watu kujiokoa. Suala hilo nalo mamlaka lilitazame.

Jambo jingine muhimu kwa magari haya ya mwendokasi ni kudhibiti idadi ya abiria.

Yanabeba watu wengi mno na ajali inapotokea inakuwa vigumu kuwaokoa hilo nalo ni jambo la kutafakari kuhusu idadi ya abiria wanaobanana kupindukia ndani ya magari hayo.

Kwa hiyo tunachotaka kusema ni hiki, kampuni hii kwa kuzingatia kilichotokea Jumapili,  itafakari upya mikakati na mifumo ya kuwaokoa abiria kwani si salama kuacha hali ikabaki kama ilivyo sasa.

Habari Kubwa