Ma-DC watatu wamsindikiza mrithi Tundu Lissu bungeni

04Sep 2019
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Ma-DC watatu wamsindikiza mrithi Tundu Lissu bungeni

MIRAJI Mtaturu ameapishwa kuwa Mbunge wa Singida Mashariki (CCM), ikiwa ni takribani saa 12 tangu Mahakama Kuu ibariki kuapishwa, huku wabunge wa Chadema wakisusa kushiriki kiapo chake.

Mtaturu aliwasili bungeni jijini Dodoma jana, asubuhi, akisindikizwa na wapambe 244 kutoka jimboni, ikiwamo Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Singida na Wakuu wa Wilaya za Ikungi, Manyoni na Singida Mjini.

Mbunge huyo mpya aliingia kwenye ukumbi wa Bunge majira ya saa 3:05 asubuhi mara tu baada ya wimbo wa Taifa kuashiria kuanza kwa mkutano wa 16 wa Bunge la 11, akisindikizwa na baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisha kula kiapo cha uaminifu mbele ya Spika Job Ndugai.

Wakati mbunge huyo akiingia ukumbini, wabunge wote wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hawakuwamo ukumbini, ikiwa ni ishara ya kususa kushiriki kiapo cha mbunge huyo. Kulikuwa na wabunge wachache wa Chama cha Wananchi (CUF) wakati wa kiapo hicho.

Mtaturu alitangazwa mshindi wa kiti cha ubunge wa Singida Mashariki (CCM) baada ya wagombea kutoka vyama vya upinzani kutorudisha fomu za kuwania ubunge wakati wa mchakato wa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.

Kiti cha ubunge wa jimbo hilo, kilitangazwa kuwa wazi na Spika Ndugai Juni 28, mwaka huu, akieleza kuwa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu (Chadema), amepoteza nafasi ya kuendelea kuwa mbunge kutokana na utoro bungeni na kushindwa kujaza fomu za tamko la mali na madeni.

Hata hivyo, Lissu kupitia kaka yake, Alute Mughwai, alifungua kesi Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo. Katika kesi hiyo, Lissu aliiomba mahakama kuzuia Mtaturu kuapishwa bungeni na kubatilisha uamuzi wa kuvuliwa ubunge.

Juzi usiku, Mahakama Kuu iliruhusu Mtaturu kula kiapo bungeni huku ikitarajia kutoa uamuzi wake kuhusu maombi ya Lissu, Agosti 9, mwaka huu.

Lissu yuko Ubelgiji akiendelea na matibabu ya kibingwa baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akijiandaa kushuka kwenye gari nyumbani kwake Area D mjini Dodoma Septemba 7, 2017.

AULIZA SWALI

Mtaturu alipata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza wakati wa kipindi cha 'Maswali', akihoji sababu za serikali kutotoa Sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya mradi wa kuchimba visima na kama serikali iko tayari kutoa Sh. bilioni mbili ili kutengeneza miundombinu ya jimbo lake kwa kuwa tathmini ilishafanyika.

Kutokana na swali hilo, Spika Ndugai aliitaka Wizara ya Maji kuhakikisha tatizo la maji katika Jimbo la Singida Mashariki linatatuliwa.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema: "Kwa kuwa Mtaturu ni jembe, wembe kutokana na kazi kubwa alizofanya, wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki, wamtumie vizuri. Serikali itatua tatizo hilo."

Katika swali la msingi, Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule 'Prof. Jay' (Chadema), aliitaka serikali kulieleza Bunge hatua inazochukua kuhakikisha inatatua changamoto ya upatikanaji wa maji jimboni kwake.

Habari Kubwa