Zahera agoma kuivaa Mbao, TFF yamfungia

04Sep 2019
Shufaa Lyimo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Zahera agoma kuivaa Mbao, TFF yamfungia
  • ***Pia yeye na Masau Bwire walimwa faini, mwamuzi aliyekataa bao la Ruvu Shooting naye afungiwa...

WAKATI Kocha Mkuu wa Klabu ya Yanga, Mwinyi Zahera, akigoma kabisa kucheza mechi za kirafiki na timu za Ligi Kuu, katika kambi yao ya Mwanza kujiandaa na mchezo wao wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United ya Zambia-

-pia amekutana na rungu la Kamati ya Bodi ya Ligi Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, ambayo imemfungia mechi tatu na kumpiga faini.

Yanga ilipanga kucheza mechi kadhaa ikiwa kambini Mwanza, mojawapo ikiwa dhidi ya Mbao FC, lakini Zahera amegomea mechi hizo kwa kuhofia wachezaji wake kuumizwa na kudai hilo lilitokea pia wakati walipocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania kuelekea mechi yao dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Akizungumza na Nipashe jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Klabu ya Yanga, Saady Khimji, alisema Zahera ameweka wazi kwamba hawezi kukubali timu yake icheze na timu kubwa mkoani humo, kwa kile anachodai huwa zinawakamia bila kuelewa wanakwenda kucheza mchezo wa kimataifa.

Makamu huyo alisema awali walipanga kukutana na Mbao FC lakini kocha amesema anahofia wanaweza kuumiza wachezaji wao kama ilivyokuwa wakati walipocheza dhidi ya Polisi Tanzania.

"Zahera amekaa na kamati ya mashindano akatupa hoja zake tukakubaliana kwa pamoja kwa sababu anasema tulipocheza na Polisi Tanzania Kilimanjaro walitukamia sana mpaka kuumiza vibaya wachezaji wetu wawili.

"Kocha amesema bora acheze na timu za Ligi Daraja la Kwanza ambazo zitacheza nao zikiwa zinajiandaa kupanda Ligi Kuu na sisi tutacheza kwa tahadhari kubwa," alisema Saady.

Wakati huo huo, Kamati ya Bodi ya Ligi Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake cha Septemba 2, mwaka huu ilipitia matukio mbalimbali ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2019/2020 iliyoanza rasmi Agosti 24, 2019 na kufanya maamuzi mbalimbali.

Katika mechi namba tisa- ambayo Yanga ilikubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting, Mwamuzi Msaidizi, Janeth Balama amefungiwa miezi mitatu kwa kushindwa kutafsiri sheria, hivyo kusababisha akatae bao halali lililofungwa na Ruvu Shooting katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Uhuru Agosti 28, mwaka huu, adhabu hiyo ikitolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.

Kocha wa Yanga, Zahera ametozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kuvaa mavazi yasiyo nadhifu na ya heshima katika mechi hiyo, kinyume cha Kanuni ya 14(2m) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu dhidi yake imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 41(13) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha.

Kadhalika, Zahera amefungiwa kuiongoza timu yake katika mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom kwa kutoa shutuma na kejeli kwa Bodi ya Ligi katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi dhidi ya Ruvu Shooting. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 41

Huku Klabu ya Yanga ikipewa onyo kali kwa kushindwa kuhakikisha Zahera anaongoza benchi la ufundi la timu yake akiwa katika mavazi nadhifu na ya heshima. Adhabu dhidi ya klabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Naye Mkurugenzi wa Ruvu Shooting, Masau Bwire ametozwa faini ya Sh. 200,000 (laki mbili), kwa kuingia ndani ya uwanja (eneo la kuchezea) baada ya filimbi ya mwisho, kinyume cha Kanuni ya 14(10) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu dhidi yake imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Habari Kubwa